AUDIO: RUGE MUTAHABA AWAKATA MAINI WANAOTEGEMEA KUBEBWA KWENYE MUZIKI …Hip Hop, Dansi, Taarab zatakiwa kubadilika …amsifu Isha Mashauzi kwa kuonyesha njia
MMOJA wa wakurugenzi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba amesema suala la nyimbo kupigwa kwenye radio yao ya Clouds FM, sio jambo la kisiasa au hisani bali ni wanachojali wao ni ubora wa kazi ya msanii.

Akiongea katika kongamano la Jukwaa la Sanaa la Basata lililofanyika Jumatano asubuhi, Ruge alisema kamwe hawawezi kupiga nyimbo mbovu na zisizo na mvuto.

Katika kongamano hilo lililofanyika ofisi za Basata, Ilala jijini Dar es Salaam, Ruge akafafanua kuwa muziki ni biashara na si siasa hivyo wasanii wanaotoa nyimbo mbovu wasitegemee kubebwa.

“Ili tupate wasikilizaji wengi ni lazima tuwe na program nzuri na muziki mzuri. Tukipata wasikilizaji wengi ndivyo tunavyozidi kupata matangazo mengi ya biashara,” alisema Ruge na kusisitiza kuwa katika hilo hawawezi kupiga nyimbo eti tu kwaajili ya kuleta usawa kwa kila aina ya muziki.

Ruge akaongeza kuwa muziki ni ‘bidhaa’ inayotakiwa kubadilika mara kwa mara ili kwenda sambamba na mahitaji ya soko la wakati husika.

“Hivi kama Cocacola ni ile ile miaka yote lakini chupa yake inabadilishwa kila baada ya miaka michache, kwanini muziki usibadilike kwa kuchomoa vionjo kutoka sehemu tofauti tofauti?” alihoji Ruge.

Bosi huyo wa Clouds akasema muziki wa Hip Hop, Dansi na Taarab unahitaji kubadilishwa ili uende na wakati.

“Kwa upande wa taarab nampongeza sana Isha Mashauzi ambaye ameweza kubadilika na kugusa vionjo vyote. Sisemi kuwa wengine hawafanyi vizuri lakini ukweli ni kwamba wanatakiwa kubadilika,” alisema Ruge.

Aidha, Ruge alikosoa mifumo ya bendi za dansi kwa kujaza wasanii wengi kwenye bendi moja, urefu wa nyimbo zao, udhaifu wa kuandaa kumbukumbu na wasifu wa kazi zao pamoja na kuwa nyuma katika matumizi yenye tija ya mitandao ya kijamii.

Ruge pia aliweka wazi kuwa yeye ni mpinzani wa maonyesho ya bure kwa vile yanashusha thamani ya msanii.

Hakuishia hapo, Ruge pia alitaka mfumo wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ubadilishwe ili uweze kuwa wa kibiashara zaidi.

SIKILIZA KIPANDE CHA SEHEMU TU YA MADA NDEFU ILIYOTOLEWA NA RUGE.

No comments