AYA 15 ZA SAID MDOE: BADO TUNAMGOMBEA BITCHUKA WA LEO? SHIKAMOO MUZIKI WA DANSI!!


ANGA ya muziki wa dansi imechafuka kidogo, hususan ile ya bendi zetu kongwe – Sikinde na Msondo, sababu kubwa ni mwimbaji mkongwe Hassan Rehani Bitchuka.

Juu ya nini? Ni juu ya tetesi kuwa mwimbaji huyo yuko mbioni kuihama Sikinde na kurejea Msondo Ngoma. Hii itakuwa ni mara yake ya tatu kuitumikia Msondo kama tetesi hizo zitatimia.

Mashabiki wa bendi hizo wamekuwa wakipigana vijembe kwenye mitandao ya kijamii, wengine wakijaribu kuonyesha kuwa Bitchuka ni muhimu sana huku upande mwingine ukimchukulia nyota huyo kama mwanamuziki wa kawaida tu.
Ukweli ni kwamba Bitchuka si mwimbaji wa mchezo mchezo, ni mmoja ya watu wenye sauti adimu katika muziki wa kiafrika, sauti iliyopasua anga kwa ubora wa hali ya juu katika miaka isiyopungua 20.

Lakini ni wazi kuwa mwimbaji huyu aliyeanza  kung’ara katika muziki wa dansi zaidi ya miaka 35 iliyopita hafanani tena na Sikinde na Msondo.

Bitchuka wa leo alipaswa kuwa na kijibendi chake mwenyewe kilichosheni vijana, bendi itakayomfanya amalizie kwa utulivu maisha maisha yake ya kimuziki yaliyobakia.

Sioni kama ni sahihi kwa Bitchuka kuendelea kupiga danadana za Sikinde na Msondo, sioni kipya kitakachobadilika katika maisha yake kupitia bendi hizo - Bitchuka alishavuna zamani sana katika Msondo, Sikinde na OSS, hakuna mavuno mapya tena.

Bitchuka wa leo wala hahitaji kutumia nguvu nyingi kuingia studio kurekodi nyimbo mpya zaidi ya kuendelea ‘kula bata’ kwa tungo zake za zamani ambazo angeweza kuzifanyia remix kidogo na kuzitumia kwenye bendi yake anayoimiliki mwenyewe.

Bitchuka wa leo alipaswa kushirikishwa kwenye kazi za vijana wa muziki wa kizazi kipya ambao wako kwenye mfumo mzuri wa kibishara utakaomsaidia mzee wetu huyo kula bingo japo kupitia miito ya simu (ring tone).


Napata ukakasi pia na mwelekeo wa muziki wa dansi kama bendi hizi kongwe zitaendelea kugombea wanamuziki wakongwe ambao wako ukingoni mwa ubora wao na pengine hata ukingoni mwa uwezo wao wa kusimama majukwaani kwenye show za kila wiki.

Ningefurahi zaidi kama bendi hizi zingekuwa zinapimana ubavu katika kusajili damu mpya ya muziki wa dansi …Huwa nacheka mwenyewe kuona mwanamzuki mwenye umri wa miaka 35 na kuendelea ndani ya Msondo au Sikinde anachukuliwa kama damu mpya, kijana, chipukizi. Duh kazi ipo.

Hata mashabiki wa Msondo na Sikinde wanaopigana vijembe juu ya Bitchuka wananiduwaza sana, hebu mwacheni mzee wa watu amalizie maisha yake vile atakavyo halafu nyinyi muwe  chachu ya kusaka vipaji vipya mitaani …Saidieni bendi zenu kutafuta kina Bitchuka wapya.

Mkiamini kuwa bendi zenu haziwezi kwenda bila kina Bitchuka, Dede na wakongwe wengine mtakuwa mnakaribisha mawazo mgando ambayo yatazidi kuzidumaza bendi na muziki wa dansi kwa ujumla wake.

Katika kipindi hiki ambacho umma wa wapenda muziki ni vijana zaidi, si sahihi sana kuwekeza katika wakongwe peke yake, bali njia nzuri ni kuwekeza kwa kuwachanganya magwiji hao na wasanii wa kizazi kipya.

Bila kufanya hivyo kazi za wazee wetu hawa zitabakia kuwa historia tu zinazoingia sikio la kulia na kutokea la kushoto kwa vijana wa leo na wa kesho na ndiyo maana najiuliza mwenyewe: “Bado tunamgombea Bicthuka wa leo?” kisha najisemea kimya kimya: “Muziki wa dansi ni ule ule, wasanii wale wale!” .. Shikamoo muziki wa dansi.

No comments