Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: CHAZ BABA PUNGUZA ‘NDONDO’ ULINDE HESHIMA YAKO

on

HAKUNA ubishi kuwa safari ya Chaz Baba kurejea Twanga Pepeta
haizuiliki, ni suala la muda tu kabla hatujashuhudia  ‘talaka rejea’ hii ikipata ufumbuzi.
Chaz Baba ameisusa bendi yake ya Mashujaa kwa karibu nusu mwaka, ukaibuka
mgogoro wa kimkataba kati ya pande hizo mbili ambao haujulikani utamalizwa
lini.
Ili kipaji chake kisipotee, Chaz Baba analazimika kutembelea maonyesho
ya bendi kadha wa kadha na kupanda jukwaani kusalimia kisanii, hatua ambayo
mimi binafsi naona inaweza ikamdidimiza badala ya kumsaidia.
Binafsi namkubali sana Chaz Baba na namuona kama mmoja wa waimbaji na
watunzi bora wa dansi la kizazi kipya ambao wanaweza kwenda sambamba na kasi ya
vijana wa Bongo Fleva …Kwangu mimi baada ya utawala wa kina Ally Chocky,
Mwinjuma Muumin na  marehemu Banza Stone,
namuona Chaz Baba ndiye mbadala namba moja.
Lakini Chaz Baba anajivurugia kwa kuonekana kirahisi kwenye maonyesho
ya bendi zingine kila wiki, anatufanya tumkinai kirahisi, anatufanya tumuone wa
kawaida.
Pengine naweza nikalazimika kumvumilia katika pita pita yake kwenye
maonyesho ya bendi zingine lakini kamwe siwezi kumwelewa kwa namna
anavyohudhuria show za Twanga Pepeta kwa kasi ya ajabu.
Kama kweli Chaz Baba ana mpango wa kurejea Twanga Pepeta, basi kwa
muda huu aliogope jukwaa la bendi hiyo kama ukoma.
Kwa kuendelea kuonekana kwenye majukwaa ya Twanga Pepeta, maanake ni
kwamba hata siku itakayotangazwa kuwa Chaz Baba anarejea nyumbani, hakutakuwa
na kipya cha kuteka hisia za watu.
Nani atakayeshtuka kusikia Chaz Baba karejea Twanga wakati kivitendo
alishaonyesha wazi mwelekeo wake. Nani atakayekuwa na ‘mshawasha’ wa kwenda
kushuhudia utambulisho wake ilhali kila wiki anaonekana kwenye maonyesho ya
bendi hiyo.
Kwangu mimi Chaz Baba si sahihi kuhudhuria maonyesho ya Twanga
kwasababu anapoonekana tu ni lazima wanamuziki wenzake wamkaribishe jukwaani.
Atakataa? Thubutu! Anahofia kuonekana ana nyodo.
Nina uhakika Chaz Baba akifuatilia kwa makini pesa anazotunzwa na
mashabiki kwenye majukwaa ya Twanga Pepeta, atabaini kuwa zinapungua badala ya
kuongezeka kadri anavyozidi kuzoeleka katika maonyesho ya bendi hiyo.
Msanii unatakiwa uwe ghali, uwe adimu, ukikubali kujirahisi na
kuonekana kirahisi sehemu za starehe, utakuwa unaishusha thamani yako bila
kujijua.
Najua Chaz Baba anaipenda sana Twanga Pepeta na ndiyo maana siku ya
sherehe ya harusi yake, maharusi waliporuhusiwa wakapumzike, akatoka kiguu na
njia yeye na mkewe na shela lake hadi Mango Garden kwenye show ya Twanga badala
ya kwenda kuufaidi usingizi wa kwanza wa siku ya kwanza ya ndoa yao.
Lakini pamoja na mahaba hayo aliyonayo, Chaz Baba anapaswa kuepuka
maonyesho ya Twanga Pepeta ili kulinda heshima ya usajili wake ujao.
Bila kufanya  hivyo wanamuziki
wenzake watamuona wa kawaida, mashabiki watamuona wa kawaida, mabosi wake wapya
watamuona wa kawaida na mwisho wa siku dau lake la usajili litakuwa la kawaida
na utambulisho wake pia utakuwa wa kawaida.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *