HEMBA ASEMA ATAIBOMOA MSONDO BITCHUKA AKIITOSA SIKINDE

KUFUATIA tetesi kwamba huenda mwimbaji mkongwe Hassan Bitchuka akajiunga na Msondo Ngoma Music Band, kiongozi mwandamizi wa Mlimani Park “Sikinde Ngoma ya Ukae”, Abdallah Hemba ameamua kufunguka na kutema cheche.

Hemba amesema kuwa anavyoamini ni kwamba Bitchuka hana mpango wa kujiunga na Msondo Ngoma, lakini hata hivyo akafika mbali na kusema kuwa kama itatokea akaenda kwa mahasimu wao hao, atafanya maamuzi magumu.

“Iwapo Bitchuka atakwenda Msondo basi nami nitakuwa tayari kuuza hata kiwanja changu ili nijibu mapigo kwa kumng’oa mwanamuziki wao yeyote wanayemtegemea,” amesema Hemba, mwimbaji kiraka na mwenye sauti nzito ndani ya Sikinde.


Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na minong’ono ya chini kwa chini kuwa huenda Bitchuka akaitosa Sikinde na kuibukia Msondo, hasa baada ya kuonekana mara kadhaa kwenye shoo za bendi hiyo iliyo chini ya Said Mabera.

No comments