HIZI NDIZO SHOW ZIJAZO ZA CHOCKY NJE YA TWANGA …Extra Bongo is loading?? Hakuna kitu kama hicho


ILE show kabambe ya Ally Chocky kutimiza miaka 30 kwenye muziki wa dansi sasa inakwenda mikoani.

Chocky ambaye katika ziara hizo hatakwenda na bendi yake ya Twanga Pepeta, atakuwa Tanga Jumamosi hii ya tarehe 10 Disemba ndani ya ukumbi wa Nyumbani Hotel.

Tarehe 30 mwezi huu, Chocky atakuwa Dodoma katika ukumbi wa Royal Village.

Akiongea na Saluti5, Chocky akasema zipo pia show zitakazofanyika mkoani Morogoro katikati ya mwezi Disemba lakini maongezi na waandaaji bao hayajakamilika.

Mwimbaji huyo amesema atapiga ‘live’ kwa kushirikiana na wasanii mbali mbali wa dansi ambao wanazifahamu nyimbo zake.

Saluti5 kwa mara nyingine tena ilimuuliza Chocky kama hii ni sehemu ya mpango wa kuirejesha Extra Bongo kwa mlango wa uani lakini mwimbaji huyo alikanusha vikali.

“Hakuna kitu kama hicho, ninauheshimu mkataba wangu na Twanga Pepeta, sina mpango wa kufufua Extra Bongo kwa staili hiyo,” alisema Chocky na kuongeza kuwa haya anayoyafanya ni sehemu ya makubaliano yake na Twanga Pepeta.

No comments