“JIAMINI” YA ISHA MASHAUZI YACHAGULIWA KUWA WIMBO BORA WA MWAKA TK FM …Amerudi ya Malaika yashika namba 2, FM ya 3, Twanga ya 8WIMBO “Jiamini” wa Isha Mashauzi umechaguliwa kuwa wimbo bora wa mwaka na wasikilizaji wa kituo cha radio cha TK FM (Tanga Kunani) cha Tanga.

Isha ameshinda taji hilo baada ya kuweka rekodi ya kukaa kwenye nafasi ya kwanza ya chati za Afro Dance kwa wiki 12 mfululizo.

Katika mjumuisho wa mwaka mzima wa 2015 uliofanywa na kituo hicho namba moja mkoani Tanga, “Jiamini” ikashinda nafasi ya kwanza huku ikifuatiwa na “Amerudi” ya Malaika Band.

Mwendeshaji wa kipindi hicho mahususi kwa muziki wa kiafrika, Dj Rogiekiess ameiambia Saluti5 kuwa “Jiamini” imetia fora kwa kuombwa mara nyingi.

Kwa mujibu wa chati za kipindi hicho kinachoruka kila siku saa 2 usiku hadi 4 usiku, wimbo wa FM Academia “Dada Wewe” umeshika nafasi ya tatu huku JB Mpiana akichukua nafasi ya nne kupitia wimbo wake “Je Ne Te Calcule Pas” wakati TOT Band wakitesa nafasi ya tano na “Wivu”.

Werrason Ngiama yuko nafasi ya sita na kitu “ Mipende” na nafasi ya saba imekwenda kwa Dar Musica na wimbo wao “Chozi la Masikini”.

 Twanga Pepeta wamesimama nafasi ya nane kwa wimbo “Uso Chini” wakiwa wamemtangulia mzee mzima Felix Wazekwa aliyeshika nafasi ya tisa kupitia wimbo “Leopard Fimbu na Fimbu” huku Double M Plus wakikamilisha chati hiyo kwa kukamata nafasi ya 10 kwa kitu “Ganda la Muwa”.

Isha Mashauzi ambaye kiuhalisia ni mwimbaji wa taarab, anachukua nafasi hiyo ya kwanza kupitia wimbo wake huo wa rumba na kutoa somo kubwa kwa wasanii wa dansi kuwa wasipobadilika kiutunzi na kiuimbaji, basi wageni kama yeye (Isha) watawapita kama wamesimama.
Chati ya Top Ten ya mwaka 2016 ya TK FM ya Tanga
Dj Rogiekiess mwendeshaji wa kipindi cha Afro Dance cha TK FM
Isha Mashauzi shindi wa Top Ten ya Afro Dance ya TK FMNo comments