JOSE MOURINHO ASEMA KIWANGO KINACHOONYESHWA NA TIMU YAKE TANGU AJIUNGE NI KIZURI

KWA kile ambacho unaweza kusema ni kama anajiliwaza, kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amesema kuwa kiwango kinachoonyeshwa na timu hiyo tangu ajiunge nayo ni kizuri kuliko cha miaka ya nyuma.

Jumapili kikosi hicho cha Mourinho kilipata pigo baada ya mchezaji Leighton Baines kupachika mkwaju wa penati zikiwa ni dakika za mwisho na kuifanya Everton kupata sare ya bao 1-1 ikiwa nyumbani kwenye uwanja wa Goodison Park.

Hiyo ni baada ya kuwa imeshaonekana kuwa wangepata ushindi wakiwa ugenini kufuatia bao lililowekwa kimiani na straika wao mahiri, Zlatan Ibrahimovic kipindi cha kwanza.

Kwa matokeo hayo, inamaana kuwa Manchester United wameshinda mechi mbili kati ya 11 na kuwafanya kuwa nyuma kwa pointi 13 dhidi ya vinara wanaoongoza Ligi hiyo, Chelsea.

Hata hivyo, pamoja na kukabiliwa na matokeo mabaya, lakini Mourinho anachowaza ni kwamba timu hiyo kwa sasa ni nzuri tofauti na ilivyokuwa chini ya Louis Van Gaal.

“Kuna mabadiliko makubwa kwenye kiwango cha uchezaji tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita, lakini kwa sasa tatizo kubwa ni kupata matokeo mazuri,” alisema kocha huyo katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi mara baada ya mechi hiyo dhidi ya Everton.

“Na kama Ander Herrera shuti lake lisingegonga mwamba matokeo yangekuwa 2-0 na mechi ilikuwa imemalizika, hii ilikuwa ni mechi nyingine ambayo tumecheza kwa kiwango kizuri na hali ya hamasa uwanjani ilikuwa nzuri mno kwa wachezaji,” aliongeza kocha huyo.


Alisema kuwa unapocheza vibaya ni lazima utapata matokeo mabaya na hivyo wanahitaji kucheza vizuri ili waweze kupata matokeo bora.

No comments