KOCHA WA CRISTAL PALACE AJIPIGIA DEBE KWA KUSEMA YEYE NDIE MBADALA KLABUNI HAPO

LICHA ya kuwa anatakiwa kupata ushindi katika mechi, kocha aliyekalia kuti kavu katika timu ya Crystal Palace, Alan Pardew amejipigia debe akisema kuwa anavyoamini yeye ndiye mtu mbadala katika nafasi hiyo.

Kwa sasa Pardew amekaliwa kooni akitakiwa kupata matokeo ya ushindi baada ya kupoteza mechi tano mfululizo wa Ligi Kuu ambazo zimeifanya klabu hiyo kuwa juu ya mstari wa kushuka daraja kwa pointi moja.

Hata hivyo pamoja na matokeo hayo Pardew ambaye msimu uliopita aliiwezesha Palace kutinga fainali ya michuano ya kombe la FA, hana mpango wa kuondoka kwenye klabu hiyo ya Park.

“Mimi ni kocha mwenye uzoefu nimeshakaa kwenye nafasi kama hii kwa miaka mingi,” alisema juzi kocha huyo mwenye umri wa miaka 55 wakati wa kijiandaa kufunga safari ya kwenda kuikabili timu inayoshika mkia kwenye msimamo wa Ligi, Swansea City.


“Huu ni mwaka wangu wa tisa kwenye michuano ya Ligi Kuu na ningependa kufikisha wa 10 nikiwa na Palace,” aliongeza kocha huyo.

No comments