LEICESTER CITY WAENDELEA KUWA NA IMANI NA KOCHA WAO RANIERY

KLABU ya Leicester City imeonyesha hali ya kuendelea kumwamini kocha aliyewapa taji la premier la msimu uliopita, Claudio Ranieri licha ya msimu huu kutokuwa na matokeo mazuri hadi sasa.

Ranieri mwenye umri wa miaka 64, aliipaisha Leicester City katika medani ya soka la Ulaya na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa England msimu uliopita.

Kwa mujibu wa mtandao wa mabingwa hao wa premier, Ranieri atabaki na vijana wake hadi mwishoni mwa msimu wa mwaka 2020.

“Klabu ya Leicester City ina furaha kutangaza kuwa meneja wa mafanikio makubwa, Claudio Ranieri atabakia nasi hata kama hatutatwaa ubingwa msimu huu.”

“Tuna imani na meneja huyo kwa miaka mingine mine kwa ajili ya mafanikio ya The Foxies hadi Juni 2020.”

“Ni meneja wa kihistoria kwetu na tunakiri sababu ya kuendelea kumwamini kwa misimu mingine ijayo,” ilieleza taarifa hiyo.

Akinukuliwa mara baada ya kukubali kusaini kandarasi mpya, Ranieri alisema hiyo ni heshima kubwa hasa baada ya kuketi na uongozi wa klabu na kueleza matarajio mapya.

“Tunahitaji kuona tunaondoka katika hatua ya msimu uliopita hadi katika kiwango cha Ligi ya Mabingwa Ulaya.”


“Ninamwamini makamu mwenyekiti Alyawatt Srivaddhanaprabha ambaye amenihakikishia ushirikiano kwa mara nyingine.”

No comments