MAPANDE NA MAGA WAIKANA DSS BAND …waomba radhi Twanga Pepeta


MADANSA wa kiume wa Twanga Pepeta Hamza Mapande na Ishaka Idd Masamaga “Maga” wameikana bendi mpya ya DSS na kusema wao si miongoni mwa wasanii wanaounda kundi hilo.

Jumamosi iliyopita wasanii hao walishiriki utambulisho wa DSS Band katika ukumbi wa Family Bar Tabata Mbuyuni jijini Dar es Salaam wakati Twanga Pepeta ikiwa safarini mkoani Ruvuma.

Mmoja wa viongozi wa DSS, Saulo John “Ferguson”  aliwatambulisha vijana hao kama madansa wa bendi hiyo.

Wakiongea katika ofisi za Saluti5 Alhamisi jioni, Maga na Mapande wakasema wao si sehemu ya DSS bali walikwenda kuwapa kampani wasanii wenzao kwa vile bendi yao (Twanga Pepeta) ilikuwa safarini.

“Sisi tuliachwa safari …Kwa kawaida huwa hatusafiri madansa wote, hivyo tulikwenda kupiga ndondo kwenye jukwaa la DSS Band ili kujikimu, lakini haimaanishi kuwa tumejiunga nayo,” alisema Mapande huku akiungwa mkono na Maga.

“Kiofisi, sisi hatukuwa watoro, tulibaki Dar es Salaam kwa utaratibu uliondaliwa na menejimenti, tukaamini kuwa si vibaya kwenda kuwatembelea wasanii wenzetu”, alisema Maga.

Dansa huyo akaongeza: “Tunaomba radhi uongozi wa Twanga Pepeta, wanamuziki na mashabiki wa bendi kwa kuchelewa kwetu kukanusha juu ya kuhusishwa na DSS. Hatujajiunga nayo na wala hatuna mpango huo”.

Saluti5 ilipoongea na mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka juu ya madansa hao kuikana DSS Band, akasema kwa kifupi: “Suala lao linazungumzika”.

Jumanne usiku, Asha Baraka alitangaza kupitia Saluti5 kuwa wanamuziki wote wa Twanga Pepeta waliotajwa kuanzisha DSS Band wamejifukuza kazi.

Lakini kwa kitendo cha madansa hao kuikana DSS Band ni wazi kuwa tamko la Asha Baraka linaweza likabadilika hasa ukizingatia kuwa walishiriki onyesho moja tu la bendi hiyo kati ya mawili yaliyofanyika hadi sasa.  
Ishaka Idd Masamaga “Maga” (kushoto) na Hamza Mapande wakiwa katika picha ya pamoja ndani ya ofisi za Saluti5 

No comments