MOURINHO ASEMA RUKSA MORGAN SCHNEIDERLIN KWENDA WEST BROM ...asema si uungwana kumzuia kama kuna ofa sahihi


Jose Mourinho amemwambia kiungo Morgan Schneiderlin anaweza kuondoka Manchester United dirisha la usajili la mwezi Januari.

Kiungo huyo wa Ufaransa amekuwa na msimu mgumu chini ya Jose Mourinho - akiwa amecheza mechi nane tu katika mashindano yote - na sasa anawaniwa na West Bromwich Albion kwa pauni milioni 18.

Akizungumza siku ya Ijumaa kuelekea mchezo wao dhidi ya Sunderland utakaochezwa Jumatatu, Mourinho alisema: "Morgan ni mchezaji anayejitambua. Ni kijana mzuri. Mwaminifu sana na muwazi.

"Amefungua moyo wake mara kadhaa, jibu langu ni jepesi. Kama angekuwa anacheza mechi nyingi ningekuwa na haki ya kusema hakuna kuondoka.

"Kama hachezi sitakuwa na haki ya kumzuia kwenda sehemu itakayompa furaha.

"Kwa hiyo jibu langu ni kwamba kama itakuja ofa sahihi na bodi ikiona ni nzuri kwa kujenga mahusiano kwa mchezaji mzuri kama Morgan basi sitakuwa na kipingamizi".
No comments