NEYMAR ASEMA HAWEZI KUATHIRIKA KAMA ASIPOSHINDA TUZO YA BALLON D'OR

STAA wa Barcelona, Neymar ni kama kaipotezea tuzo ya mchezaji bora wa dunia “Ballon d’Or” baada ya kusema kuwa hawezi kuathirika kisoka kama hatashinda taji hilo.

Nyota huyo wa timu ya taifa ya Brazil alishika nafasi ya tano katika mbio za kuwania tuzo ya mwaka huu huku Cristiano Ronaldo akiwashinda Lionel Mess na Antoine Griezmann katika mchuano huo.

Hata hivyo, Neymar alisema jana kwamba hatakosa usingizi kama hakutwaa tuzo hiyo.

“Najisikia mwenye furaha nikiwa hapa Barcelona katika timu hii na maisha niliyonayo,” alisema nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kupitia katika tovuti ya La Liga.

“Ni kweli ni malengo yangu kutwaa tuzo ya ballon d’Or lakini siwezi kujiua kama sitafanikiwa kuitwaa,” aliongeza.


Alisema kuwa hachezi soka kwa ajili ya kutwaa ballon d’Or bali anacheza kwa sababu anaupenda mchezo huo.

No comments