RASHID PEMBE ASEMA SAMBA MAPANGALA ALIMZUIA KUJIUNGA NA MSONDO NGOMA

MKONGWE wa Domo la Bata “Saxaphone”, Rashid Pembe “Profesa” amefichua kwamba saa hizi angekuwa ni mwanamuziki wa Msondo Ngoma Music Band kama si ziara ya Samba Mapangala nchini Tanzania mwaka 2005.

Amesema kuwa aliitwa na marehemu Muhiddin Gurumo wakati huo na kumtaka akaongeze nguvu upande wa ala ya upepo baada ya afya ya Ramadhan Mnenge kuanza kuwa mgogoro lakini ilikuwa vigumu kumkubalia.

“Niliipenda Msondo na niliona heshima kutakiwa na bendi kubwa kama ile, ila bahati mbaya nilikuwa kwenye ziara ya Samba Mapangala hivyo iliniwia vigumu,” amesema Pembe.


Pembe amesema kuwa, hakuweza tena kwenda Msondo hata baada ya kumaliza ziara hiyo kwani tayari akili yake ilishalenga kwenye kufanya muziki wa mahotelini na ndipo akaanza harakati za kuanzisha Mark Band aliyonayo hadi sasa. 

"Kitu pekee nilichoweza kufanya ni kusaidia kushiriki kupiga Domo la Bata walipokuwa wanarekodi kibao "Jesca" na baada ya hapo nikaachana nao na kuendelea na hamsini zangu, ila niliipenda Msondo Ngoma," anasisitiza Pembe.

No comments