ROGART HEGGA AMJIBU KIUNGWANA ASHA BARAKA …afafanua kuhusu DSS Band na Twanga Pepeta


MWIMBAJI na mtunzi mahiri wa muziki wa dansi Rogart Hegga “Katapila” amejibu kuhusu taarifa ya ‘kutimuliwa’ kazi  Twanga Pepeta.

Jana usiku Asha Baraka aliiambia Saluti5 kuwa Rogart Hegga na Ferguson wamejifukuza kazi kwa kitendo chao cha kutangaza kuanzisha bendi yao ya DSS.

Wanamuziki hao wawili wa Twanga Pepeta pamoja na madansa Mapande na Maga walikuwa miongoni mwa wasanii waliotambulishwa na DSS Band Jumamosi usiku.

Lakini tayari Mapande na Maga wameikana DSS Band na kwenda kumwangukia bosi wao Asha Baraka kwa madai kuwa wao walienda kupiga ndondo tu.

Akizungumza na Saluti5 kwa njia ya simu, Rogart Hegga akasema hawakuanzisha DSS Band kwa nia mbaya wala hujuma, bali ni kwa lengo la kujitafutia kipato kwa siku ambazo bendi yao (Twanga Pepeta) haitakuwa na maonyesho.

“Naithamini na kuiheshimu Twanga Pepeta na ndiyo maana nilikubali kuitumikia kama kibarua, bila mkataba wowote,” alieleza Rogart.

Katapila anaeleza zaidi: “Hatukuwa na dhamira mbaya, lakini kama mama Asha Baraka ameamua kutufukuza itabidi kukubaliana na uamuzi wake.

“Hadi muda huu sijapata taarifa yoyote kutoka kwake na mimi bado naamini ni mwana Twanga Pepeta na nitaripoti kazini, kama kuna taarifa yoyote basi nitakutana nayo huko.

“Kama msimamo wake utakuwa huo nitauheshimu bila kinyongo na nitamtakia kila la kheri na pia nitakuwa tayari kumpa ushirikiano wangu muda wowote atakapouhitaji.”


Saluti5 bado inaendelea kumtafuta Ferguson ili kupata maoni yake juu ya taarifa ya Asha Baraka.

No comments