ALLY CHOCKY KUITOSA TWANGA? MFANYABIASHARA WA SONGEA AFIKA BEI


GWIJI wa muziki dansi nchini 'Kamarade' Ally Chocky inasadikiwa yuko mbioni kuitosa bendi yake ya The African Stars “Twanga Pepeta” baada kutengewa 'mkwanja' mnene na bendi ya Extra Peramiho ya mjini Songea.

Habari za uhakika kutoka mjini Songea zinaeleza, Chocky akiwa mjini humo wiki iliyopita alikokwenda kutumbuiza na Twanga Pepeta wakati wa sikukuu ya Krisimasi aliitwa mezani na tajiri wa Extra Peramiho mfanyabiashara John Floyd Ngonyani ili kuweka mambo sawa.

Taarifa zinaeleza,katika kikao hicho cha siri kilichofanyika katika moja ya hoteli za Kitalii mjini humo Chocky, alimueleza Ngonyani kuwa bado ana mkataba na Twanga Pepeta unaofikia ukomo mwakani hivyo kwake itakuwa ngumu kwake kuitosa bendi hiyo kutokana na kubanwa kisheria.

Inaelezwa mfanyabiashara huyo alimueleza Choki yuko tayari kuvunja mkataba huo kwa gharama yoyote kwani amepanga kuiimarisha Extra Peramiho kuwa moja ya bendi kubwa za muziki wa dansi nchini.

Tayari bendi hiyo imeshawanyakuwa baadhi ya wanamuziki waliowahi kufanya kazi na Chocky enzi ya Extra Bongo wakiongozwa na kiongozi Greyson Semsekwa na Bob Kisa.

Extra Peramiho pia iko mbioni kuwanasa mpiga dramu Sunday Mashine na mpiga solo Ephraim Joshua, Mfaume Solo na mpiga Tumba wa Tanzania One Theatre (TOT) Salum Chakuku 'Kuku Tumba ambao wote wamewahi kufanya kazi na Chocky.

Saluti5 ilimtafuta Ngonyani kupata ukweli wa taarifa hizo ambapo alikiri kuteta na Chocky na kusema kila kitu kitawekwa wazi mambo yatakapoiva.

Kwa upande wake Chocky alisema ni kweli aliitwa na mfanyabiashara huyo lakini ilikuwa ni kwaajili ya kutoa ushauri wa namna ya kuiboresha bendi hiyo na hafahamu habari za yeye kuondoka Twanga zinatokea wapi.

No comments