Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: DARASA UKICHEMKA ‘MUZIKI’ UTAKUPELEKA DARASANI

on

Naweza kusema kuwa zari limemwangukia mdogo wangu Darasa, msanii wa
siku nyingi kwenye muziki wa Kizazi Kipya, lakini aliyeibuka hivi karibuni tu na kupata mafanikio makubwa kupitia wimbo wake wa “Muziki”.
Nina mengi ya kumuasa Darasa katika kipindi hiki ambacho anatesa na
kibao hicho, hasa ikizingatiwa kuwa alishasota sana kwenye gemu akiwashuhudia
wenzake wakitusua, lakini hakukata tamaa.
Tangu baada ya kuachiwa kwa wimbo ” Muziki”, zimeshatoka
nyimbo nyingine nyingi za Bongofleva kutoka kwa wasanii wenye majina makubwa
zaidi yake, lakini bado mashabiki huwaambii kitu kwenye kibao hicho – Hii ina
maana nyingi lakini kubwa ni kuwa ‘kila nabii na zama zake’ – Kwamba kama Mungu
kakuandikia kutusua, basi utatusua tu.
Kwa sababu wote tunafahamu kuwa Darasa si wa jana wala juzi kwenye
muziki na ameshatoa nyimbo nyingi ambazo pengine nyingine ni kali kuliko
“Muziki” lakini hazikubahatika
kushika chati namna hii, basi kazi pekee kubwa iliyobaki kwa Darasa hivi sasa
ni kuhakikisha analinda daraja alilopanda kwa ghafla bila mwenyewe kutarajia.
Anapaswa sasa kuumiza kichwa kwelikweli, asikurupuke na kuachia nyimbo
zisizo na kiwango ambazo zinanaweza kumporomosha badala ya kumbakisha kileleni.
Wimbo huu wa “Muziki” unaweza kuwa ni ngazi ya kumpeleka Darasa kwenye
kilele cha mafanikio, lakini unaweza pia kuwa ‘jeneza’ litakalomsindikiza
kwenye safari ya kuzimika kimuziki iwapo atashindwa kuupiku yeye mwenyewe wimbo
wake huo wa “Muziki”.
Muziki hauna mwenyewe hivyo lolote linaweza kutokea kwenye gemu kama
hatokuwa makini, kwani nafasi aliyopo walishaishikilia wasanii wengi ambao hivi
sasa wamebaki kugongea fegi tu vijiweni kwa kushindwa kujipanga ipasavyo.

Kukubalika kwa wimbo “Muziki” kusimfanye abweteke kiasi cha
kuona amemaliza kila kitu katika sanaa, akumbuke kuwa bado ana deni kubwa kwa
mashabiki wake la kuhakikisha anafyatua ngoma kali zaidi kila anapozama studio
kurekodi.
Kujisahau ni kati ya magonjwa mabaya mno yanayowafanya wasanii wetu wengi
wasiweze kudumu kwenye chati kwa muda mrefu na ndo maana nasisitiza kumweleza
kuwa nafasi aliyopo walishapita wengi.
Mashabiki ni wepesi wa kukusahau na kugeukia wengine wanaofanya vyema,
hata kama nyimbo zako zilikuwa na uzuri wa namna gani ama ziliwafariji kwa
kiwango kipi, hivyo hakikisha unawalinda na kuwazuia wasikukimbie.
Majuzi nilimsikia mmlikili wa Twanga Pepeta Mamaa Asha Baraka
akimsifia radioni Darasa  na kukiri kuwa
wimbo wa “Muziki” umeuteka nchini lakini akatoa angalizo kuwa msanii huyo sasa
ana deni kubwa la kuhakikisha anatoa wimbo mkali zaidi vinginivyo atabakia kuwa
historia.
Darasa anapaswa kuangalia mahitaji ya soko kwa wakati husika na asikurupuke
kuachia wimbo mpya kwa kufuata mkumbo. Akae akijua kuwa kuna wasanii wengi waliopotea
ghafla muda mfupi tu baada ya kutoa nyimbo kali zilizobeba heshima mithili ya
wimbo wa taifa.
Anapaswa kuilinda kazi yake nzuri ambayo ni matunda yake ya ibada ya
subira na moyo alionao wa wivu wa mafanikio na tamaa ya kufika pale ambapo
wenzake wengine wanafika kila leo.
Hili pia liwe somo kwa wasanii hata wasio wa Bongofleva, maisha ya
muziki yako hivyo na msifikiri kuwa kila mwaka utakuwa mwaka wako hata kama ni
hodari wa kukesha ukitunga mistari.
Mwisho nimalizie tu kwa kusisitiza kuwa Darasa atake asitake, ni lazima
atoe wimbo bora kuliko “Muziki” vinginevyo atajerejeshwa darasani.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *