AYA 15 ZA SAID MDOE: MUZIKI WA DANSI UNAHITAJI MBINU MBADALA


RAFIKI yangu mmoja aliniambia kuwa hivi karibuni alipanda ‘bus’ kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na hakubahatika kuusikia muziki wa dansi mwanzo hadi mwisho wa safari.

Anadai nyimbo zilizotawala ndani ya basi hilo zilikuwa ni za bongofleva na taarab, hususan za Isha Mashauzi na Mzee Yussuf ingawa mara chache zilisikika pia nyimbo za injili.

Alishangaa sana na kuniuliza: “Hivi kumbe hata vyombo vya usafiri navyo vinaubania muziki wa dansi!!!? Mi nilidhani ni vyombo vya habari tu”.

Nikamwambia usiilaumu kaniki, weusi ndo rangi yake. Nikamfafanulia kuwa vyombo vya usafiri ni sehemu tu ya vyanzo vingi vinavyofuata mkumbo na kuamini kile wanacholishwa na vyombo vya habari.
Bila muziki wa dansi kuzungumzika na kuchezwa kwenye vyombo vya habari, unategemea vipi jamii ifahamu kuhusu muziki huo?

Lakini pia wanamuziki wengi wa dansi wanadhani kutunga nyimbo na kutumbuiza kwenye kumbi za starehe inatosha, hawajui kutengeneza matukio yatakayolazimisha muziki wao uongelewe, hawajui kuigeuza migogoro yao ya kikazi kuwa mtaji wa kukuza muziki wa dansi, hawajui kuwa ‘bifu’ kati ya msanii na msanii inaweza kugeuka kuwa bonge la biashara.


Miongoni mwa mambo ambayo yanachochea kushuka kwa soko la muziki wa dansi ni kile kitendo cha muziki huo kutoongelewa, kususiwa na kupuuzwa (kama nitakuwa sijatumia neno kali).

Wakati muziki wa dansi ulipokuwa ukitesa sokoni, ulikuwa ukizungumzika kila kona. Magazetini, radioni, kwenye vituo vya televisheni na hata kwenye vyombo vya usafiri pia.

Leo hii kuna mgogoro mkubwa wa Chaz Baba na Khalid Chokoraa lakini wao wenyewe na watu waliowazunguuka wameshindwa kuugeuza mgogoro huu kuwa ‘mtambo’ wa kuteka vichwa vya habari na hatimaye kupiga pesa ndefu ya show ya pamoja.

Ijumaa usiku kupitia kipindi cha Friday Night Live cha EATV kuna jambo moja lilinifariji sana kupitia muziki wa dansi … Ni kile kitendo cha kuwa na mahojiano ya mmiliki wa Twanga Pepeta Asha Baraka na wanamuziki walioasi bendi yake Rogart Hegga na Ferguson.

Unapoona maongezi ya muziki wa dansi katika kipindi kama kile ambacho kimebobea zaidi kwa mahojiano na wasanii wa bongo fleva unafarijika na kujisemea ‘Afadhali sasa muziki wa dansi umeanza kuongolewa’.

Lakini ilikuweje kipindi kile kikawasaka Asha Baraka, Rogart Hegga na Ferguson? Ni kutokana na namna chanzo cha kwanza cha habari (Saluti5) kilivyoripori kwa aina ya kuhamasisha na ‘kuilazimisha’ jamii ya wapenda muziki iione habari ile ni kubwa, iliyojaa mgogoro na inayotia hamu ya kusubiri matokeo ya kilichoripotiwa.

Na ndiyo maana hata siku ya pili baada ya Saluti5 kuandika juu ya wanamuziki hao kuanzisha kinyemela bendi yao (DSS Band),  magazeti yakaipa uzito wa juu habari hiyo. Hii ni moja ya ubunifu unaohitajika katika kulazimisha muziki wa dansi uwe gumzo.

Hata namna Saluti5 ilivyoripoti habari ya J4 Sukari wa TOT kwenda kupiga ndondo na Twanga Dodoma huku bendi yake ikiwa na kazi Dar es Salaam, ililazimisha muziki wa dansi kuongelewa kwenye vituo vingi vya radio.

Wanamuziki wa dansi wasibweteke na kutulia kama maji mtungini, tunapita katika dunia nyingine kabisa inayohitaji ubunifu na ujanja wa hali ya juu, bila hivyo wataendelea kufunikwa na bongofleva katika kila nyanja …kwa sisi tuliocheza mchezo wa draft kuna kitu huwa kinaitwa ‘force king’. Ni wakati sasa wa wanamuziki wa dansi ku – force king.

No comments