Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: TUNADUMAA KWA KULINDA VIPAJI VYA ZAMANI NA KUPUUZA VIPAJI VIPYA

on

MAJUZI Diamond Platnumz alikabidhiwa bendera ya taifa wakati akiondoka
kwenda kutumbuiza kwenye ufunguzi wa michuano ya AFCON huko Gabon. Baadhi ya wadau
wakongwe wa muziki wakanuna.
Rais Magufuli alipomfagilia Christian Bella, hali ilikuwa hivyo hivyo
pia – baadhi ya mashabiki wa muziki wa dansi wakanuna. Kisa? Eti Bella hapigi
dansi. Sijui nani aliwaambia kuwa anayepaswa kusifiwa ni mtu wa dansi tu?!
Ni heshima kubwa kwa Tanzania kwa hatua hii ya Diamond kwenda
kutumbuiza AFCON. Si jambo dogo hata kidogo, tumeshindwa kwenda huko kisoka
basi wacha Diamond akatutoe tongotongo.
Watu wa dansi wanalalamika Diamond kwenda AFCON, wanamuona ni msanii
wa kuchovya, wanaamini mwanamuziki aliyestahili kwenda Gabon ni mwanamuziki wa
dansi.
Hawataki wala hawahitaji kujua vigezo, hawana muda wa kujiuliza
Diamond kaonekana wapi hadi kachaguliwa, wamesahau kuwa wanamuziki wetu wa
dansi kwa sasa nyimbo zao kuvuka mipaka ya Tanzania ni sawa na kusubiri meli
‘airport’.
Moja ya tatizo kubwa la watu waliouzunguuka muziki wa dansi ni tabia
ya kukariri – kwamba muziki wa dansi ndio mpango mzima – muziki wa aina
nyingine hauna nafasi kwao, haufai, hauna maana!
Lakini lipo kundi lingine kubwa la watu waliouzunguka muziki wa dansi
ambao wana kasumba mbaya zaidi – eti muziki wa ukweli ni wa zamani tu – waimbaji
wa ukweli ni Salum Abdallah, Mbaraka Mwishehe, Marijani Rajab, Gurumo, Bitchuka
na wengine kama hao.
Kamwe wadau hawa hafikirii nje ya box kwamba kuna siku tutahitaji kuwa
na Salum Abdallah, Mbaraka Mwishehe, Marijani Rajab, Gurumo, na Bitchuka wapya.
Hawaamini kuwa kina Diamond, Kiba na wenzao wanaweza kuwa kina Bitchuka wapya
katika aina nyingine ya muziki.
Kumekuwa na tatizo kubwa kwenye media zetu zinazopiga muziki wa dansi
kuthamini zaidi muziki wa kale badala ya kuchochea vipaji vipya.
Nakubali ‘Ya kale ni Dhahabu, lakini ya kale hiyo inakuwa dhahabu pale
inapodimika, tunapozigeuza ‘zilipendwa’ kuwa ndiyo chakula sahihi kwa kila siku
maanake inakuwa ni muziki ule ule kwa mashabiki wale wale. Hapa tusitegemee
kuzalisha mashabiki wapya wa dansi.
Naam huwezi kuzalisha shabiki mpya wa dansi kwa kumpigia nyimbo za
zamani mtoto wa kidato cha kwanza, atakuwa anaona nyota nyota tu …katika nyimbo
kumi anaweza akailewa moja au mbili. Hata mimi binafisi katika utoto wangu
sikuwahi kuwa shabiki wa zilipendwa.
Hatari iliyopo ni kwamba watangazaji wapya wa dansi wanakuwa adimu na
hata hao wachache waliopo hawapewi ushirikiano wa kutosha kutoka kwa mashabiki
na wanamuziki wakongwe, wanaonekana hawaujui muziki wa dansi… tunataka
watangazaji wale wale, nyimbo zile zile kwa mashabiki wale wale.
Bendi zinahofia kurekodi nyimbo mpya kwa sababu hazipewi nafasi kubwa
kama za zamani, wasanii wapya wa dansi wanapatikana kwa uchache sana maana
hakuna nafasi kwenye bendi na hata zikiwepo hawatathaminiwa sana kutokana na
imani ile ile kuwa wakongwe hawana mpinzani wala mbadala.
Na hii ndio tofauti kubwa ya muziki wa bongo fleva na muziki wa dansi.
Bongo fleva inatoa muziki mpya kila kukicha, wasanii wapya kila kukicha,
maproducer wapya kila kukicha, ubunifu mpya kila kukicha, huku hali hiyo ikiwa
ni kinyume chake muziki wa dansi.
Napenda sana namna wasanii wa kizazi kipya wanavyopokezana vijiti
kuanzia enzi za kina Kwanza Unit, Hard Blasters, GWM, Mr II (Sugu), Sos B,
Afande Sele, Mr Nice hadi kizazi cha sasa hivi cha kina Diamond. Napenda namna
kunavyokuwa na ving’ang’anizi wachache ambao wanatesa sokoni kwa miaka mingi,
lakini napenda pia namna pumba zinavyojichuja… wanaibuka wasanii kumi kwa
wakati mmoja lakini saba kati yao wanapotea, watatu wanakamata soko.
Zilipendwa zina utamu wake kwa zinaowagusa, lakini shurti ziwe adimu,
hata zilipendwa ya bongo fleva inanoga kwasababu ya kuadimika kwake. Tuboreshe
soko jipya la dansi kwa faida ya kizazi cha sasa. Kama taarab inabadilika kila
kukicha, kwanini dansi ishindikane?

Comments

comments

About Saluti 5

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *