AYA 15 ZA SAID MDOE: UNAPOILAUMU ‘AFRIKA BAMBATAA’ NA KUSAHAU ‘MISAKATO’ NA ‘CLUB RAHA LEO’ UNASTAHILI POLE


SIKU moja nilikuwa namtazama Mzee wa Upako  Anthony Lusekelo kupitia moja ya vituo vya televisheni, akanikuna pale aliposema ‘Huwezi kutoa nazi Mbeya na kuja kuziuza Dar es Salaam’.

Naam nazi chimbo lake ni Dar es Salaam  na mikoa mingine ya pwani. Nazi zinapaswa kutoka Dar es Salaam na kwenda kuuzwa Mbeya, ukifanya kinyume chake unajitafutia hasara ya kujitakia. Ni sawa na kutoa mahindi Dar kisha ukayauze Mbeya.

Hata muziki ni kama nazi au mahindi, soko lake linabadilika kutegemeana na wakati na eneo, unapaswa kujua unaupanda lini na wapi na kisha ujue sehemu sahihi ya kwenda kuuza.

Muziki wa bendi (dansi) kwangu bado ndiyo muziki bora zaidi kwa hapa nyumbani Tanzania lakini ni wazi kuwa soko lake limeyumba zaidi ya sana kuanzia majumbani mwetu, kwenye vyombo vya habari hadi katika kumbi za starehe.

Nenda club za disco uone namna bongo fleva inavyochuana vikali na ngoma za nje, lakini unaweza usibahatike kabisa kumsikia dj akigonga nyimbo za dansi japo kwa kuteleza. Muziki wa dansi katika baadhi ya maeneo umekuwa sawa na kutoa nazi Mbeya na kuja kuziuza Dar es Salaam.

Majuzi wasanii wawili wa kizazi kipya (Roma na Darasa) wameujaza hadi kufuru ukumbi wa Dar Live lakini marapa zaidi ya 10 wa bendi za dansi (hapo hapo Dar Live) walishindwa hata kufikia robo ya kile walichovuna Roma na Darasa. Hili ni anguko kubwa.

Siku hizi mashabiki wa dansi wanatazama bendi ukumbini kama vile wako jumba la sinema …hakuna kucheza ni kutazama tu, lakini taarab mashabiki wanacheza. Anguko lingine hili.


Kwa bahati mbaya sana katika anguko hili lawama nyingi zimepelekwa kwa vyombo vya habari hususan radio na moja ya kituko cha karne ni zile shutuma zinazopelekwa kwa kituo cha Clouds FM kwa kukiua kipindi cha Afrika Bambataa ambacho kilifanya vema sana katika kulisongesha mbele gurudumu la muziki wa dansi.

Naweza nikaunga mkono kuwa vyombo vya habari vimechangia kuushusha muziki wa dansi kwa kiasi fulani, lakini kamwe siwezi kuunga mkono kuwa  Afrika Bambataa imeondoka na muziki wa dansi.

Vipi kipindi kimoja, kituo kimoja kiwe muuaji wa muziki wa dansi? Haiingii akilini …kwanini hatujiulizi kuhusu RTD (TBC) na vipindi vyake kibao vilivyokuwa vinapiga muziki wa dansi. Vimepotelea wapi? kwasababu gani?.

Kipindi cha Misakato kilikuwa kipindi bora cha kutuletea nyimbo mpya za dansi kila wiki, Club Raha Leo Show ilitupa raha kwa kumimina uhondo ‘live’ kutoka katika moja ya bendi zetu. Viko wapi hivi vipindi? Siku hizi Club Raha Leo imekuwa chombo cha kusaka vipaji (Talent Search). Anguko lingine la muziki wa dansi.

Zamani kupitia RTD ulikuwa unalisikia dansi tangu saa 12 asubuhi, unajiandaa kwenda shule huku unakula dansi kupitia kipindi cha “Kumekucha” baadae unasindikizwa na kipindi cha “Asubuhi Njema”, kisha mchana unapiga ugali wako huku unapata ngoma tamu za dansi kupitia kipindi cha “Mchana Mwema”, jioni utakutana na “Jioni Njema” usiku utakumbana na “Usiku Mwema” kote huko  ni dansi tu, hakuna taarab, kwaya wala muziki wa nje ya nchi.

Viko wapi vipindi hivi vitamu vya RTD (TBC)? Kwanini hatuilaumu RTD? Kwanini hatusemi RTD imeua dansi? Ni wazi kuwa hata chombo hicho cha umma kimeamini kuwa kinahitaji kubadilika na kwenda na soko la sasa. Kinahofia kutoa nazi Mbeya na kuja kuziuza Dar es Salaam.

Tuendelee kutafuta sababu za kisayansi za kurejesha ubabe wa muziki wa dansi na tuachane na sababu za kisiasa, tutambue kuwa vyombo vya habari vinajiendesha kibiashara na kamwe havitakuwa na muda wa kuipa mbeleko aina fulani ya muziki kama haina manufaa kwenye biashara yao.

Wakati tukiilamu Afrika Bambataa ya Clouds FM na kusahau Misakato na Club Raha Leo ya RTD, hebu tujiulize inakuweje msaniii mmoja wa bongo fleva anauza show kwa shilingi milioni tano huku bendi kubwa ya dansi yenye wanamuziki 25 ikiuza show kwa milioni moja?

No comments