AYA 15 ZA SAID MDOE: UTAWALA WA NYOSHI NA ABUU SEMHANDO NI MFANO WA KUIGWA


Awali ya yote nimtakie mapumziko ya amani Abuu Semhando kwenye nyumba yake ya milele, sasa ni miaka sita na siku kadhaa tangu mwanamuziki huyo wa Twanga Pepeta afariki dunia kwa ajali ya pikipiki Disemba 17, 2010.

Nadiriki kusema kuwa Abuu Semhando “Babu” aliyekuwa akizicharaza drums za Twanga Pepeta, ameondoka na sehemu kubwa ya ladha ya muziki wa bendi hiyo.

Abuu Semhando alikuwa ‘mpishi’ mzuri wa Twanga Pepeta, aliyesimama kwa msimamo thabiti kuhakikisha mabadiliko ya ‘ingia toka’ ya wasanii mbali mbali ndani ya Twanga hayapotezi utambulisho wa bendi hiyo.

Lakini pia ni ukweli usiopingika kuwa Abuu Semhando ameondoka na nusu ya nidhamu iliyokuwa inapatikana Twanga Pepeta kuanzia mazoezini hadi kwenye maonyesho.

Semhando alikuwa kiongozi shupavu asiyekubali kuyumbishwa kitaaluma na mtu yeyote. Aliweza kujenga na kutetea hoja mbele ya waandishi wa habari, mashabiki, maofisa wenzake wa bendi na hata kwa wamiliki wa bendi.

Nakumbuka siku moja mwaka 2010, nilipewa zigo na wamiliki wa bendi kumshawishi Abuu Semhando juu ya mwimbaji mmoja nyota aliyekuwa mbioni kujiunga na Twanga Pepeta.

Wamiliki na baadhi ya wanamuziki waandamizi walishatia tiki mwimbaji huyo atue Twanga Pepeta lakini Abuu Semhando alikataa kata kata kwa kusema nyota huyo hafanani na ‘rangi’ ya Twanga Pepeta. Nikakabidhiwa jukumu la kumshawishi Semhando.

Nilikutana na Semhando na kumpa sera zangu nilizoamini kuwa zitafanikiwa kumgeuza mawazo, lakini wapi! Sikufanikwa. Jamaa alinisomesha vilivyo, akanipa mapungufu mengi ya mwimbaji huyo kiumbaji, kinidhamu (hususan ulevi wa kupindukia) na tabia yake ya kutotulia kwenye bendi moja. Mwimbaji yule hakufanikiwa kutua Twanga Pepeta.


Huyo ndiye Abuu Semhando aliyeifanya Twanga Pepeta inyooke, Semhando aliyeheshimika na kuogopewa na wanamuziki wote, Semhando aliyefanya utoro na uchelewaji uwe bidhaa adimu mazoezini na kwenye maonyesho ya bendi hiyo.

Abuu Semhando naweza kumlinganisha na Nyoshi el Saadat wa FM Academia, ni watu wanaofanana sana kikazi. Nidhamu ya woga kwa walio chini yao na juu yao, ni msamiati mgumu kwao.

Nyoshi na Semhando ndiyo waliokuwa chachu ya upinzani wa Twanga Pepeta na FM Academia, aina ya uongozi wao na vijembe walivyokuwa wakipeana kwenye vyombo vya habari, ilikuwa ni burudani tamu inayopatikana nje ya jukwaa.

Wakati Abuu Semhando alipokuwa akijivunia uzalendo na kuwataka mashabiki waiunge mkono Twanga Pepeta kwa madai kuwa ndiyo inayopiga muziki wa Kitanzania, Nyoshi aliwataka wapenzi wa muziki wasibabaike na madebe kwa kisingizio cha uzalendo.

Nyoshi alisisitiza kuwa muziki upo FM Academia na kwamba Twanga Pepeta wanapiga madebe …hakuna muziki. Kauli hii ilimtia hasira Semhando, hasira za kimuziki, hasira za kutaka kuthibitisha kuwa wao hawapigi madebe, hasira zilizopelekea kuzalishwa kwa nyimbo tamu kutoka bendi zote mbili …Twanga Pepeta na FM Academia.

Ama kwa hakika Semhando na Nyoshi walizalisha upinzani mzuri baina Twanga na FM, upinzani ambao ulifanya soko la bendi hizo liwe juu kupita maelezo.

Kama ilivyokuwa kwa Abuu Semhando ambaye hakuwa mtu wa kuzurura ovyo, Nyoshi pia ni mtu adimu anayejua kuilinda thamani yake, huwezi kumuona kirahisi mitaani, kwenye mabar au katika kumbi za starehe. Binafsi naamini ili muziki wa dansi uendelee, wanahitajika kina Nyoshi na Abuu Semhando wengi.

No comments