BAADA YA UKIMYA WA MIAKA 20, BURUDANI KUREJEA TENA KATIKA UKUMBI WA SAFARI RESORT KIMARA …FM Academia ‘kuuzindua’ Januari 28


Ukumbi maarufu  wa Safari Resort ulioko Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam, utazindua upya shughuli za burudani Jumamosi ya tarehe 28 mwezi huu kwa dansi la ‘kufa mtu’ kutoka kwa FM Academia “Wazee wa Ngwasuma” (pichani juu).

Safari Resort unaomilikiwa na mfanyabiashara Hugo Kisima, ulisimamisha shughuli za burudani tangu mwaka 1996 na kubakia na huduma ya vinjwaji na chakula tu (Bar), lakini sasa utamu unarejea upya baada ya ukarabati wa aina yake.

Ukumbi huo uliojengwa mwaka 1970 ulikuwa ukumbi wa nyumbani wa bendi ya Maquis du Zaire kabla mmiliki wa ukumbi hajaanzisha bendi yake ya Orchestra Safari Sound (OSS) iliyoweka kambi ya kudumu hapo na kutikisa jiji la Dar es Salaam.

Hugo Kisima ameiambia Saluti5 kuwa baada ya tarehe 28, burudani zitakuwa zikiendelea kila wikiendi.

Mfanyabiasha huyo ambaye pia aliwahi kumiliki klabu ya soka ya Safari Contractors, amesema siku hiyo ya ufunguzi wa burudani ndani Safari Resort, wataalikwa watu mbali mbali wakiwemo wamiliki wa bendi za dansi, taarab na vikundi vya sanaa, wamiliki wa kumbi za starehe, waandishi wa habari, wafanyakazi na wanamuziki wa zamani wa bendi zilizokuwa zikipiga hapo bila kusahau wanasoka wa iliyokuwa Safari Contractors.

Habari njema ni kwamba Hugo Kisima ameshawalipia kiingiilio mshabiki wote watakaoenda Safari Resort kushuhudia onyesho la FM Academia ...yaani hakutakuwa na kiingilio mlangoni.


No comments