BIRTHDAY YA MIAKA KUMI YA JAHAZI MODERN TAARAB YAJA DARLIVE

SHEREHE ya kutimiza miaka kumi tangu kuanzishwa kwa bendi ya mipasho ya Jahazi Modern Taarab imeandaliwa ambapo imepangwa kufanyika februari 25, ndani ya Darlive Mbagala Zakheem, jijini Dar es Salaam.

Bosi wa Jahazi Modern, Hamis Boha ameitonya Saluti5 kuwa anaamini sherehe hiyo itakuwa funika bovu kutokana na maandalizi ambayo bado wanaendelea kuyafanya.

Boha amesema burudani kemkemu zinatarajiwa kupamba birthday hiyo ambayo wasanii mbalimbali waliowahi kufanyakazi na Jahazi Modern wamealikwa kuhudhuria.

“Tumeandaa zawadi nyingi ambazo tutazitoa kwa wasanii na wadau wetu mbalimbali ambao wameonyesha kuwa pamoja nasi tangu kuanzishwa kwa Jahazi Modern,” amesema Boha.

Jahazi Modern inayotumia mtindo wa ‘Nakshinakshi’ imeanzishwa rasmi Desemba 21, mwaka 2006 na baadhi ya wasanii waliojiengua kutoka Zanzibar Stars Modern Taarab, ambao baadhi yao Leyla Rashid, Khadija Yussuf na Mzee Yussuf aliyeamua kumrejea Mungu hivi sasa.


Wasanii wengine wa mwanzo ndani ya Jahazi Modern ni Fatma Shobo, Isha Mashauzi, Miriam Amour, Fikirini Urembo, Rashid Yusuph, Babu Ally na Mussa Mipango.

No comments