BOSI WA BARCELONA ALIYEMKANYAGIA LIONEL MESSI AVULIWA MADARAKA

KUFUATIA maoni aliyoyatoa kwamba Lionel Messi anabebwa na wachezaji wenzake, Barcelona imemfukuza kazi meneja uhusiano wa klabu hiyo, Pere Gratacos.

Taarifa ya klabu imefafanua kuwa maamuzi hayo yamefanywa kwa sababu Gratacos alitoa maoni binafsi ambayo hayaendani na msimamo wa klabu.

“Bila ya (Andres) Iniesta, Neymar, Pique na wengine, Messi asingekuwa mchezaji mzuri kiasi hiki,” Gratacos aliwaambia waandishi wa habari baada ya upangaji wa droo ya robo fainali ya Kombe la Mfalme ambayo barca walipangiwa timu ngumu ya Real Sociedad.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa maamuzi hayo yamefanywa na Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona, Albert Soler ambaye kuanzia sasa atashika nafasi iliyoachwa na Gratacos.

Hata hivyo, Barcelona imesema Gratacos ataendelea kufanya kazi ndani ya klabu hiyo lakini katika nafasi tofauti za chini katika akademi ya La Masia.


Gratacos aliwahi kuifundisha Barcelona B kuanzia 2013-15 na akiwa mchezaji alishindwa kupanda kutoka Barcelona B kuja Barcelona A na akacheza pia Osasuna na Figueres.

No comments