JOSE MOURINHO AMKINGIA KIFUA "MBORONGAJI" POGBA... asema si lazima abebeshwe zigo la lawama

PAUL Pogba, mwanasoka ghali zaidi duniani alikuwa na usiku mbaya dhidi ya Liverpool Jumapili iliyopita.

Aliushika mpira ndani ya boksi mbele ya refa Michael Oliver na kuwapa Liverpool penati iliyozaa bao la kuongoza.

Na alikuwa na bahati kutotolewa kwa kadi nyekundu pale alipomkaba kooni Jordan Henderson na kumbwaga chini kama mwanamieleka wa WWE.

Haikuwa mara ya kwanza kwa Pogba kuchemka uwanjani katika mechi dhidi ya timu kubwa.

Wakati hakuna shaka kuhusu uwezo wake kwenye kiungo kwamba amechangia United kucheza mechi 16 bila kupoteza, amekuwa “akipotea” uwanjani dhidi ya wapinzani wao wa Top 4; Chelsea, Tottenham, Arsenal, Manchester City na sasa Liverpool.


Hata hivyo, kiungo huyo ambaye amefunga magoli sita na amenyoa staili sita tofauti za nywele tangu atue United, ametetewa na kocha wake, Jose Mourinho kwamba “Si lazima mchezaji mmoja ang’ae na abebeshwe mzigo wote mabegani kwake. Muhimu kila mtu kikosini acheze vyema.”

No comments