LICHA YA KUISAWAZISHIA ARSENAL, MASHABIKI WAMZODOA GIROUD KWA KUSHANGILIA SARE


LICHA ya kuisawazishia Arsenal dakika za majeruhi, mshambuliaji Olivier Giroud ameshutumiwa vikali na mashabiki wa timu hiyo.

Giroud analaumiwa kwa kupoteza muda baada ya kufunga bao la kusawazisha, ambapo badala ya kuwahi kuchukua mpira na kuupeleka kati, yeye akawa kwenye kilele cha furaha kwa kushangilia kwa staili ya 'scorpion kick'.

Arsenal ilitoka nyuma 3-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Bournemouth na kuchomoa magoli yote huku Giroud akifunga la tatu katika dakika ya pili kati ya sita zilioongezwa kufidia muda uliopotea.

Mshambuliaji huyo wa Kifaransa akatumia sekunde kadhaa kukumbukia bao lake la 'scorpion kick' alilofunga dhidi ya Crystal Palace.

Wakati Alex Oxlade-Chamberlain anaokota mpira na kumpigia kelele wakimbie kati huku Gabriel akithubutu hata kumvuta jezi, Giroud alikuwa bize kuhakikisha anamalizia 'sherehe' yake ya kufurahia goli mbele ya mashabiki wa Arsenal waliokuwa ugenini.

Mashabiki wa Arsenal wanamshutumu Giroud huku wakiamini kuwa bado walikuwa na uwezo wa kushinda mchezo iwapo muda usingepotea kizembe baada ya bao lao la kusawazisha.

No comments