MAJERUHI LUKA MODRIC, MARCELO WAONGEZA PRESHA REAL MADRID

HOFU kubwa imeongezeka Real Madrid kwamba kuumia kwa Marcelo na Luka Modric ni mwanzo tu wa majanga katika klabu hiyo.

Ratiba ngumu inazidi kushika kasi na kocha Zinedine Zidane atakuwa na wakati mgumu kupanga kikosi chake katika mechi yao ya leo ya marudiano ya robo fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya Celta Vigo ambayo itazima ndoto zao kama hawatapindua ugenini matokeo ya kipigo cha 2-1 walichopata nyumbani katika mechi yao ya kwanza kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu wiki iliyopita.

Zidane alizungumzia masikitiko yake kufuatia kuumia kwa nyota wake Modric na Marcelo katika mechi dhidi ya Malaga ambao watakuwa nje ya uwanja kwa mwezi mzima, huku tayari wakiwa na majeruhi Dani Carvajal, Gareth Bale, Pepe na James Rodriguez.


Huku Madrid ikiandamwa na adhabu ya kufungiwa na FIFA kusajili, Zidane ana mtihani mkubwa wa kuendeleza mafanikio yao baada ya hivi karibuni kuiongoza timu hiyo kucheza mechi 40 bila kupoteza.

No comments