MASHAUZI CLASSIC WAJA NA ISHA’S NIGHT FEBRUARI 9 … ni ule usiku wa Isha wa kuonyesha ‘mapafu’ yake ya mbwa


Ule usiku wa Isha Mashauzi (Isha’s Night) unaofanyika kila mwaka, umewadia tena na safari hii ni Alhamisi ya Februari 9 ndani ya Mango Garden Kinondoni.

Ni nyesho ambalo humpa nafasi Isha Mashauzi kusherehekea siku yake ya kuzaliwa huku akipewa uwanja mkubwa wa kuonyesha uwezo wake wa kukamua jukwaani kwa muda mrefu bila kupumzika.

Ni usiku ambao Isha Mashauzi husimama jukwaani kwa zaidi ya saa mbili mfululizo na kupiga nyimbo zake zote kali.

Ndio onyesho pekee ambalo watu humshuhudia Isha akiimba zaidi ya nyimbo nane mfululizo kitu ambacho hakijawahi kufanywa na mwimbaji yoyote wa taarab, awe wa kiume au wa kike. Ni Isha tu hakuna ubishi katika hilo.

Katika onyesho hilo la aina yake, Isha akiwa na kundi lake la Mashauzi Classic, watasindikizwa na Siza Mazongela mamaa wa Segere.

Ikumbukwe kuwa Siza ndiye mtu wa kwanza kukifichua kipaji cha Isha Mashauzi kabla hajapokewa na Mzee Yussuf.

Onyesho hilo pia litakuwa linamifikisha Isha katika miaka 11 ya uimbaji.
Isha Mashauzi ameiambia Saluti5 kuwa siku hiyo pia itakuwa ni maalum kwa wote waliozaliwa mwezi Ferbruari “Team Februari”.

Mkurugenzi wa Saluti5 Said Mdoe naye amezaliwa mwezi Februari japo ni katika tarehe tata - (Ferbruari 29) ambayo mwaka huu ataisikia kwenye bomba tu.

No comments