Habari

MATUKIO MAKUBWA YA MUZIKI WA DANSI NCHINI KWA MWAKA 2016

on

Mchambuzi wa muziki wa dansi William
Kaijage (Papaa Kaijage)
anashuka na ripoti kamili ya matukio makubwa ya
muziki wa dansi kwa mwaka 2016.
BENDI MPYA
•Tarehe 26-Feb-2016, bendi mpya ya BMM yazinduliwa rasmi katika ukumbi
wa Mzalendo Pub. Bendi hiyo, pamoja na wanamuziki wengine, inaundwa na Mule
Mule FBI (Rais wa bendi) na Totoo Ze Bingwa. Bendi pia inamjumuisha mpiga solo
mahiri Losso Mukenga, ambaye pia ni mpiga solo wa Ally Kiba. Hata hivyo bendi
hii ilidumu kwa mchache sana.
•Tarehe 08-Apr-2016 (Ijumaa), bendi mpya ya Sky Melodies chini ya
uongozi wa Nicco Millimo, yatambulishwa ndani ya Club la Aziz Classic, Dodoma.
•May-2016, bendi mpya ya Ivory Band yaanzishwa. Bendi hii kwa asilimia
kubwa imeanzishwa na wanamuziki waliotokea bendi ya Double M Plus baada ya
kutokea mtafaruko. Wanamuziki hawa ni kama Dogo Rama, Saleh Kupaza, Jojo
Jumanne, Rashid Sumuni na kadhalika.
•Nov-2016, bendi ya Original Dar Musica yaanzishwa chini ya
mwanamuziki Jaddo Field Force. Hii ni baada ya mwanamuziki Jaddo Field Force
kuenguliwa (au kujiengua) katika bendi ya Dar Musica.
•Tarehe 24-Dec-2016 (Jumamosi), bendi mpya inayoitwa DSS Band
(Dar-es-Salaam Super Sound) “Wazee wa Kujilipua” yazinduliwa rasmi katika
ukumbi wa Family Bar, Tabata Mbuyuni. Bendi hiyo inamilikiwa na wanamuziki
Ferguson na Rogart Hegga “Caterpillar”.
UZINDUZI WA ALBUM MPYA
•Tarehe 28-May-2016, bendi ya Twanga Pepeta yazindua album ya
“Usiyaogope Maisha” katika jiji la Mwanza kwenye ukumbi wa Villa Park. Hii ni
album ya 13 tokea Twanga Pepeta ianzishwe. Ni album ya kwanza ya Twanga Pepeta
kuzinduliwa nje ya Dar-es-Salaam.
•Tarehe 16-Sep-2016 (Ijumaa), bendi ya Dar Musica, chini ya uongozi wa
Jaddo Field Force “FFU”, yazinduliwa upya (relaunching) na kuzindua album mpya
ya “Chozi la Maskini” yenye nyimbo 6 katika ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni.
Uzinduzi huo umesindikizwa na Malkia wa Mipasho Khadija Kopa na Msondo Ngoma.
•Nov-2016, bendi kongwe ya Mlimani Park Orchestra “Sikinde-Ngoma ya
Ukae” yazindua album ya “Jinamizi la Talaka” katika ziara ya kanda ya ziwa,
Geita (Ijumaa tarehe28-Oct-2016 ),Kilimanjaro Hotel Nyegezi Mwanza (Jumamosi
tarehe 29-Oct-2016) na Kahama, Shinyanga (Jumapili tarehe 30-Oct-2016).
•Tarehe 23-Dec-2016 (Ijumaa), Talent Band chini ya uongozi wa Hussein
Jumbe yazindua album ya “Kipima Joto” katika ukumbi wa Kisuma, Temeke
Mwembeyanga.
KILI MUSIC AWARD
•Kwa mara ya kwanza baada ya karibia miaka 20, mwaka 2016 tukio la
Kili Music Award lashindwa kufanyika kutokana na sababu nyingi tofauti.
•Tarehe 10-Dec-2016 (Jumamosi), lilifanyika tukio la EATV Award ambayo
haikushirikisha kipengele chochote cha muziki wa dansi.
WANAMUZIKI (NA WADAU WAKUBWA) WA MUZIKI WALIOFARIKI
•Tarehe 20-Feb-2016 (Jumamosi), mchambuzi mahiri wa muziki wa dansi na
mtangazaji wa Tumaini Radio, Fred Mosha afariki dunia katika hospitali ya
Muhimbili kutokana na maradhi ya saratani. Azikwa tarehe 22-Feb-2016 (Jumatatu)
katika makaburi ya Kinondoni.
•Tarehe 25-Feb-2016 (Alhamis), Kassim Mapili akutwa nyumbani kwake
Tabata akiwa amefariki. Mara ya mwisho kuonekana inasemekana ilikuwa usiku wa
tarehe 23-Feb-2016 (Jumanne) alipotoka kuangalia mechi ya Arsenal na Barcelona.
Azikwa tarehe 26-Feb-2016 (Ijumaa) katika makaburi ya Kisutu.
•Tarehe 23-Mar-2016 (Jumatano), mwanamuziki Ismail Selemani Kizunga
afariki dunia akiwa Kilosa, Morogoro. Kizunga alikuwa mwanamuziki mahiri katika
upigaji gitaa la kati (rhythm guitar) na gitaa la solo.
•Tarehe 09-Apr-2016 (Jumamosi), mwanamuziki Ngongo Onawembo Ndanda
“Ndanda Cosovo Kichaa” afariki dunia katika hospital ya Muhimbili kutokana na
maradhi ya vidonda vya tumbo.
•Tarehe 27-May-2016 (Ijumaa), mdau mkubwa wa muziki wa dansi na ambaye
kwa kipindi kifupi cha mwaka 2000 aliwahi kuwa mmiliki wa bendi ya FM Academia,
Hussein Macheni, afariki dunia.
•Tarehe 15-Jul-2016 (Ijumaa), mpiga drums wa Akudo Impact Mpogoro
“Mashine” Chitalula afariki dunia kutokana na tatizo la figo.
•Tarehe 07-Oct-2016 (Ijumaa), Mama Salome Kiwaya , mmiliki wa bendi ya
Saki Stars ya Dodoma afariki dunia katika ajali ya gari. Saki Stars ni bendi
inayoongozwa na mwanamuziki Yamodo. Mama Salome Kiwaya alikuwa pia Mwenyekiti
wa Umoja wa Wanawake (UWT)-CCM Mkoa Dodoma.
•Tarehe 20-Oct-2016 (Alhamis), Mzee Omary Kungubaya afariki dunia.
Mzee Kungubaya ndiye aliyetunga na kuimba (huku akipiga gitaa lisilotumia
umeme) wimbo wa “Ugua Pole” ambao ulikuwa maarufu kwa kuwa kiashirio (signature
tune) cha kipindi cha wagonjwa kupitia RTD (Radio Tanzania Dar-es-Salaam)
almaarufu kama “Salamu kwa Wagonjwa”.
•Tarehe 21-Dec-2016 (Jumatano) jioni, mpiga trumpet wa bendi ya Msondo
Ngoma Music Band Roki Malekela afariki dunia katika hospitali ya Mwananyamala.
WANAMUZIKI WAKUBWA WALIOHAMA BENDI
•Tarehe Feb-2016, wanamuziki James Kibosho (mpiga drums) na Hosea
Mgohachi (mpiga bass) warejea Twanga Pepeta. Wanamuziki Kabatano na J4
wajiengua na kujiunga na TOT Plus. Mwingine aliyejiengua ni mpiga drums Chenga.
•Tarehe 08-Mar-2016, rapa Fergusson na mnenguaji Super K watangazwa
rasmi kujiunga bendi ya Twanga Pepeta. Wanamuziki hawa watambulishwa rasmi
tarehe 19-Mar-2016 (Jumamosi) katika ukumbi wa Mango Garden. Bendi ya Twanga
Pepeta yatangaza kuwaondoa kwenye kikosi wanamuziki Rama Pentagon, rapa J4 Sukari,
mpiga tumba Kaposhoo na madansa Mandela, Dogo White na Said Aset.
•Tarehe 30-Apr-2016 (Jumamosi), mwanamuziki Saad Ally “Machine”
aliyekuwa Msondo Ngoma ajiunga rasmi na bendi hasimu ya Mlimani Park Orchestra
“Sikinde Ngoma ya Ukae”. Alitambulishwa rasmi siku ya mpambano wa Sikinde na
Msondo uliofanyika TCC Chang’ombe. Baadaye alipelekwa kwa mkopo kwenye bendi ya
Talent Band ya Hussein Jumbe.
•May-2015, wanamuziki Dogo Rama, Salehe Kupaza, Jojo Jumanne, Ramadhan
Sumuni na Amina Juma wajiengua Double M Plus na kuanzisha Ivory Band.
•Tarehe 04-Jun-2016, mwanamuziki Khalid Chokoraa ambaye alikuwa mmoja
wa wakurugenzi wamiliki wa bendi ya Mapacha Watatu ajiengua rasmi na kuhamia
bendi ya Twanga Pepeta kwa utambulisho uliofanyika katika kiwanja cha Leaders
Club.
•June-2016, mwanamuziki Raja Ladha aiacha Mashujaa Band na kujiunga na
bendi ya Dar Musica. Anakuwa mwanamuziki mwingine wa Mashujaa Band kujiunga na
Dar Musica baada ya Pansia Budansi. Hii ikafuatiwa na wanamuziki wa Mashujaa
Band Jimmy, mpiga solo Proper, mpiga tumba Dulla Ngoma, mpiga drums Emma
Chocolate na mpiga keyboard Fred Manzaka pia kujiunga na Dar Musica. Baadaye
mwezi wa Sep, Dar Musica wakamchukua mpiga drums Sele Kadanse kutoka Ivory
Band.
•Jul-2016, mwanamuziki Adam Mbombole ajiunga na Malaika Music Band ya
Christian Bella. Mwanamuziki Montana Amarula ajiunga na Mashujaa Band.
•Aug-2016, mpiga bass Jojo Jumanne arudi Twanga Pepeta akitokea Ivory
Band.
•Sep-2016, rapa Totoo Ze Bingwa arejea bendi ya Malaika Music Band
chini ya Christian Bella.
•Nov-2016, mwanamuziki King Blaise ajiondoa bendi ya FM Academia na
kuanzisha bendi yake inayoitwa East African Ngwasuma Band “Wazee wa Kampa Kampa
Tena” yenye makazi yake Mererani, Arusha.
•Nov-2016, mwanamuziki Jaddo Field Force aondoka (au aondolewa) kutoka
bendi ya Dar Musica. Aanzisha bendi nyingine ya Original Dar Musica.
MATUKIO MENGINE MAKUBWA
•Tarehe 17-Feb-2016 (Jumatano), Chama cha Muziki wa Dansi (CHAMUDATA)
chafanya uchaguzi wa viongozi wapya katika ukumbi wa Polisi Band, Kilwa Road,
Dar-es-Salaam. Viongozi waliochaguliwa ni Juma Ubao “King Makusa” (Mwenyekiti),
Lt Col Mwandike (Makamu Mwenyekiti), Hassan Msumari (Katibu) na Anna Mwaole
(Katibu Msaidizi). Walichaguliwa pia wajumbe 15 wa kamati ya utendaji na 63 wa
halmashauri kuu.
• Feb-2016, Shirikisho la Muziki wa Dansi Nchini lafanya uchaguzi wa
viongozi ambapo Addo November Mwasongwe alichaguliwa kuwa mwenyekiti.
•Tarehe 18-Mar-2016 (Ijumaa), bendi ya Double M Plus (zamani Double M
Sound) yafanya utambulisho wa ujio mpya ndani ya Mango Garden wakiwa na
wanamuziki wapya Saleh Kupaza na Dogo Rama.
•Tarehe 21-Mar-2016 (Jumatatu), Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye, akutana na wadau wa muziki wa dansi katika ukumbi wa
Vijana Social Hall, Kinondoni
•Tarehe 16-Apr-2016 (Jumamosi), bendi ya Twanga Pepeta ndani ya ukumbi
wa Mango Garden wafanya tukio la “Usiku wa wa Pongezi-Twanga Pepeta Jana na
Leo”
•Tarehe 28-Apr-2016 (Alhamis), Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam, Paul
Makonda, akutana na wadau mbalimbali wa muziki (dansi, taarabu etc) na wamiliki
wa kumbi za burudani katika ukumbi wa Vijana Social Hall, Kinondoni kujadili
sheria ya kusitisha muziki saa 6 usiku.
•Tarehe 30-Apr-2016 (Jumamosi), bendi za Mlimani Park Orchestra
“Sikinde Ngoma ya Ukae” na Msondo Ngoma zafanya mpambano ndani ya ukumbi wa TCC
Chang’ombe chini ya udhamini wa Radio One, NSSF na benki ya Posta.
•Tarehe 01-Jun-2016 (Jumatano), bendi ya Msondo Ngoma yafanya tukio la
“Msondo Family Day” katika ukumbi wa TCC Chang’ombe (CDS Park). Tukio la
“Msondo Family Day” lafanyika pia Jumapili tarehe 31-Jul-2016 (katika ukumbi wa
DDC Kariakoo), tarehe 27-Aug-2016 (DDC Kariakoo), Ijumaa tarehe 30-Sep-2016
(Mango Garden), Jumamosi tarehe 29-Oct-2016 (Lekham Hotel Buguruni), Ijumaa
tarehe 02-Dec-2016. Katika ukumbi wa Lekham Hotel Buguruni (Jumamosi tarehe
29-Oct-2016) walifanya pia sherehe ya kutimiza miaka 52 tokea bendi
ilipoanzishwa mwaka 1964. “Family Day” ya mwisho kwa mwaka 2016 ilifanyika
Ijumaa ya tarehe 02-Dec-2016 ambapo ilimtamulisha mpiga saxophone nguli Luza
Elias aliyepata kupiga bendi kadhaa ikiwemo Simba Wanyika.
•Tarehe 03-Jun-2016 (Ijumaa), Rais wa Shirikisho la Muziki Nchini,
Addo November Mwasongwe katika ukumbi wa Maelezo atangaza kumteua John Kitime
kuwa Katibu Mkuu Mpya wa Shirikisho hilo (akichukua nafasi ya Abdul Salvador
“Father Kidevu”)
•Tarehe 04-Jun-2016 (Jumamosi), Mwanamuziki Christian Bella afanya
show maalum katika kiwanja cha Escape One kusherehekea miaka yake 10 ya muziki
Tanzania.
•Jun-2016, bendi ya Mapacha Watatu yabadili jina na kuwa MAPACHA MUSIC
BAND. Hii ni siku chache baada ya mmiliki mwenza Khalid Chokoraa kujiunga na
bendi ya Twanga Pepeta.
•Tarehe 06-Jul-2016, bendi za Mlimani Park Orchestra “Sikinde” na
Msondo Music Band wakutana kwenye show ya pamoja iliyofanyika siku ya Eid
al-Fitr kwenye ukumbi wa Dar Live, Mbagala.
•Tarehe 30-Jul-2016 (Jumamosi), lafanyika tukio linaloitwa “Tanzania
Band Festival” (Tamasha la Bendi la Tanzania) katika kiwanja cha Leaders Club
lililoandaliwa na kampuni ya Q Plus. Mgeni rasmi wa tukio hilo alikuwa mkuu wa
mkoa wa Dar-es-Salaam, mhe Paul Makonda. Bendi 14 zilihusika ambazo ni Le
Capitale “Wazee Sugu” (King Kiki), Top Band (TID), B Band (Banana Zorro), QS
International Band, TOT Plus, Mapacha Watatu, Family Team, Mlimani Park
Orchestra “Sikinde”, Msondo Ngoma, Skylight Band, Akudo Impact, Yamoto Band,
Twanga Pepeta na FM Academia.
•Tarehe 27-Aug-2016 (Jumamosi), mnenguaji Lilian Internet astaafu
rasmi unenguaji baada ya miaka 17 ya kuwa jukwaani kwa kufanyiwa sherehe maalum
ya kumuaga kwa show maalum ya Twanga Pepeta iliyofanyika katika ukumbi wa Mango
Garden.
•Tarehe 24-Sep-2016 (Jumamosi), ilikuwa ni kilele cha “Siku ya Msanii”
iliyofanyika katika Kijiji cha Makumbusho. Kutoka saa asubuhi hadi saa 12 jioni
kulikuwa na burudani za muziki wa dansi, taarab, DJ, Bongo Flava, Ngoma Asilia,
Muziki wa Injili, Sanaa za Mikono, Uchoraji, Uchongaji na kadhalika. Tuzo
mbalimbali zilitolewa.
•Tarehe 26-Nov-2016 (Jumamosi), mwanamuziki Ally Choki afanya tukio la
kukumbuka miaka 30 tokea anze kazi ya muziki mwaka 1986. Tukio lilifanyika
katika ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni ambalo lilisindikizwa na Msondo Ngoma,
Komandoo Hamza Kalala, Zahir Ally Zorro, Tshimanga Kalala Assossa, Msaga Sumu
na Twanga Pepeta.
•Tarehe 27-Nov-2016 (Jumapili), bendi ya Mlimani Park Orchestra
yafanya tukio la “Usiku wa Sikinde” katika ukumbi wa DDC Kariakoo.
•Tarehe 25-Dec-2016 (Jumapili) siku ya Christmas, wafanyika mpambano
wa ma-rapper katika ukumbi wa Dar Live Mbagala. Baadhi ya walioshiriki ni
Kalidjo Kitokololo “Kuku”, Sauti ya Radi, Papy Catalogue, G7, J4, Khalid
Chokoraa, Kabatano na Hitler. Hakukuwa na mshindi kwa vile nusu fainali yake
itafanyika siku nyingine katika ukumbi wa Mango Garden.
•Tarehe 25-Dec-2016 (Jumapili) siku ya Christmas, tukio ambalo
lingejumuisha bendi 7 za muziki wa dansi na taarab (Mlimani Park-Sikinde,
Msondo Music Band, FM Academia, Jahazi Modern Taarab, East African Melody,
Ogopa Kopa na Wakali Wao Modern Taradance) lililopangwa kufanyika Morogoro
katika uwanja wa Jamhuri lashindwa kufanyika kutokana na bendi kutolipwa malipo
yaliyobakia na waandaaji (Tegemeo Arts).
•Tarehe 31-Dec-2016 (Jumamosi), mpambano wa bendi za Mlimani Park Orchestra
“Sikinde” na Msondo Music Band uliokuwa ufanyike katika viwanja vya TCC
Chang’ombe washindwa kufanyika kutokana na zuio la kesi iliyopo mahakamani ya
wakazi/majirani wa TCC Chang’ombe kuhusiana na upigaji muziki eneo hilo.

IMECHAMBULIWA NA WILLIAM KAIJAGE  (PAPAA KAIJAGE)

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *