ROGART HEGGA ASEMA DSS BAND HAIRUDISHI MPIRA KWA KIPA …wakanusha kujisalimisha Twanga


MMOJA wa viongozi wa kundi jipya la muziki wa dansi - DSS Band, Rogart Hegga “Katapila” amesema wamejipanga vizuri na hawana mpango wa kurudisha nyuma majeshi.

Rogart Hegga na Ferguson mwishoni mwa mwezi uliopita waliamua kuanzisha bendi hiyo kwa lengo la kujiongezea kipato, lakini hatua hiyo ikapelekea wote wawili kutimuliwa Twanga Pepeta.

Awali wasanii hao walisema DSS Band ingekuwa bendi yao ya pembeni ambayo wangekuwa wanaitumikia siku ambazo Twanga Pepeta haina maonyesho, lakini sasa wameamua kokomaa na kuisuka kiushindani bendi yao mpya.

Akiongea na Saluti5, Rogart Hegga alisema wamesikitishwa sana na habari iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku kuwa wamejisalimisha Twanga Pepeta na kurejea kundini.

“Hatuna mpango wa kujisalimisha, tunakuja na nguvu kamili kupitia DSS Band na tunaomba mashabiki wetu wasiyumbishwe na habari za propaganda,” alisema Rogart.

“Ukimya wetu ulikuwa ni kwaajili ya kukamilisha taratibu za usajili wa bendi pamoja na kutengeneza nyimbo mpya. Wiki ijayo tutaanza rasmi program zetu,” anafafanua zaidi Rogart Hegga.

Aidha, Rogart Hegga amesema wiki ijayo pia wataweka wazi kikosi kamili cha DSS Band ambacho kiko kambini.

No comments