SADIO MANE AIPELEKA SEGAL ROBO FAINALI KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA

MSHAMBULIAJI mahiri wa Liverpool, Sadio Mane sio tu alifungua akaunti kwenye ushindi wa Senegal “Lions of Teranga” dhidi ya Zimbabwe, lakini aliiwezesha kuwa nchi ya kwanza kutinga robo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2017.

Katika mchezo huo, Zimbabwe walioianza michuano ya mwaka huu kwa kishindo wakiwalazimisha sare ya mabao 2-2 miamba ya soka Algeria, walijikuta wakichezea kichapo cha mabao 2-0.

Mane alianza kuifungia Senegal bao la kuongoza dakika ya tisa kwa shuti kali la mbali akiunganisha krosi ya mshambuliaji wa Lazio ya Italia, Keita Balde Diao.

Dakika nne baadae Henri Saiver anayekipiga kwa mkopo St. Etienne ya Ufaransa akitokea Newcastle United, akafunga bao la pili kwa mpira wa faulo wa zaidi ya mita 20.


Kwa ushindi huo Lions of Teranga walijihakikishia kutinga robo fainali wakifikisha pointi sita kwa michezo miwili wakiongoza Kundi B wakifuatiwa na Tunisia wenye pointi tatu, Algeria na Zimbabwe kila mmoja akiwa na pointi moja hivyo hazina nafasi ya kuing’oa hata ikipoteza mechi ya mwisho dhidi ya Algeria.

No comments