SERENA WILLIAMS ATWAA TAJI LA SABA AUSTRALIA OPEN NA KUWEKA REKODI

SERENA Williams amemshinda dada yake, Venus kwa seti mbili mfululizo na kutwaa taji lake la saba la Australian Open na kuweka rekodi ya zama za mashindano ya wazi kwa kutwaa taji la 23 Grand Slam.

Serena, 35, jana alishinda kwa seti 6-4-6-4 na kumpita Steffi Graf katika rekodi ya ushindi wa mataji mengi zaidi tangu mashindano ya Grand Slam yakubali kushirikisha wachezaji profeshenali mwaka 1968.

Gwiji wa Australia, Margarat Court aliyetwaa mataji 24 kwa zama zote ndie mchezaji pekee aliyemzidi serena katika mashindano ya Grand Slam.

“Hongera Serena kwa kubeba taji la 23,” alisema Venus ambaye kwa kucheza akiwa na umri wa miaka 36 ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mkongwe zaidi kucheza fainali ya Australia Open katika zama za mashindano ya wazi.

Serena alimsifu dada yake ambaye alicheza jana fainali kwa mara ya kwanza ndani ya miaka nane akisema: “Nisingeweza kufikisha mataji hayo 23 bila ya yeye. “Hamna namna ningekuwa Na.1 bila yeye, yeye ndie mwongozo wangu.”


“Yeye ni sababu pekee ya mimi kusimama hapa leo. Yeye ni sababu pekee tunaitwa “Williams Sister’s”. asante kwa ushawishi wako kwangu. Kila siku ulivyokuwa unashinda wiki hii nilijiona nimeshinda pia.”

No comments