TEVEZ AVUNJIWA NYUMBA NA WEZI SIKU YA HARUSI YAKE

WEZI walivunja na kuingia katika nyumba ya aliyekuwa mshambuliaji wa Manchester City, Carlos Tevez viungani mwa mji wa Bueno Aires nchini Argentina Jumapili na kuiba wakati nyota huyo alipokuwa nchini Uruguay kufunga ndoa.

Maafisa wa polisi wanasema kuwa Tevez hakuwasilisha ripoti kuhusu wizi huo, hivyo basi haijulikani ni nini alichoibiwa.
Polisi wanasema kwamba waligundua kuhusu wizi huo siku ya Jumanne baada ya kuwaona wanahabari wamekusanyika nje ya nyumba ya nyota huyo wa Argentina.

Wanasema kuwa wezi wengi waliingia katika nyumba hiyo ambayo Tevez na familia yake walikuwa wamekodi huku wakisubiri nyumba yao ambayo ilikuwa inafanyiwa ukarabati.

Inadaiwa wezi hao waliingia nyumba hiyo kupitia eneo ambalo ukarabati huo ulikuwa ukifanywa.

Baada ya Tevez kuarifiwa kuhusu wizi huo, alirudi nyumbani kwake kwa helkopta na kukuta mlango wa nyumba yake uko wazi huku vitu vikiwa vimepekuliwa.


Tevez baadae alisafiri kuelekea Mexico kama alivyopanga kwa fungate yake na mpenziwe wa utotoni Vanessa Masilla.

No comments