XAVI ATOA USHAURI WA BURE KWA MESSI, INIESTA NA KOCHA WAO LUIS ENRIQUE

NAHODHA wa zamani wa timu ya Barcelona, Xavi ni kama kawapa ushauri Lionel Messi Andres Iniesta na kocha wao, Luis Enrique baada ya kusema kuwa angependa kuona wanaendelea kuitumikia klabu hiyo hata baada ya msimu huu kumalizika.

Kauli ya staa huyo imekuja baada ya kuwepo kwa hali ya wasiwasi kuhusu hatma ya nyota wa timu ya taifa ya Argentina, Messi kuendelea kuwa katika mabano baada ya kutofanyika mazungumzo ya kumpa mkataba mpya ili aweze kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya Camp Nou.

Kwa sasa mkataba wa Iniensta na klabu hiyo umebakiza mwaka mmoja na nusu, huku taarifa kutoka nchini Hispania zikidai kuwa Barca tayari imeshapata mrithi mbadala wa Luis Enrique ambaye ameshakataa kuweka wazi kama ataongeza mkataba wake ambao unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Hata hivyo, Xavi ambaye alitwaa mataji matatu msimu uliopita akiwa na klabu hiyo ukiwa ni msimu wa kwanza wa Luis Enrique wa 2014/15, ana matumaini watatu hao wanatakiwa kueleza hatma yao kabla ya msimu huu kufikia ukingoni.

“Ningependa kuona Iniesta, Messi na Luis Enrique wakiwa pamoja msimu ujao,” staa huyo aliuambia mkutano wa waandishi wa habari.


“Hii itakuwa na maana kwamba Barca itaendelea kuwa na afya njema,” aliongeza.

No comments