ARSENAL, CHELSEA WAINGIA VITANI KUWANIA SAINI YA WINGA WA ATLETICO MADRID

VIGOGO vya soka vya England, Arsenal na Chelsea vimo katika kupigana vikumbo kumwania winga wa Atletico Madrid, Yannick Carrasco.

Winga huyo mwenye umri wa miaka 23, amekuwa hana namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Atletico na sasa anahusishwa kutaka kuondoka katika La Liga.

Tayari kocha wa Atletico, Diego Simeone amenukuliwa akikiri kutomtumia mara kwa mara winga huyo, lakini amekanusha kutaka kumruhusu ahame.

Hadi sasa Carrasco amepachika jumla ya mabao 10 katika La Liga msimu huu na Chelsea chini ya meneja Antonio Conte imeshaliweka jina la mwanandinga huyo katika orodha ya usajili wake wa majira ya kiangazi.

Pamoja na Conte kuweka bayana azma hiyo, kocha Arsene Wenger wa washika mitutu wa London amekiri hatua ya kumwania kama njia ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji.

Kwa mujibu wa The Sun, klabu hizo zote mbili zimetuma maombi ndani ya Atletico, huku zikianza pia mazungumzo ya awali na Carrasco.

Hata hivyo, winga huyo amebainisha mapenzi aliyonayo ya kutaka kucheza katika timu itakayomwamini katika kikosi cha kwanza kwa kile alichokisema anataka kutunza kiwango chake cha kisoka.


Kutokana na mazingira hayo, klabu ya Chelsea ina nafasi kubwa ya kupata saini ya Carrasco kutokana na ukweli kuwa Diego Costa yumo katika hatihati ya kutaka kutimkia nchini China.

No comments