ARSENE WENGER AKANA KUWA KATIKA MPANGO WA KUMSAJILI KIPA JOE HART

BOSI wa washika mitutu wa jiji la London, Arsene Wenger ameweka bayana kuwa hana mpango wa kumsainisha mlinda mlango wa zamani wa Manchester City, Joe Hart.

Joe Hart kwa sasa anadakia timu ya Torino ya nchini Italia inayoshiriki Ligi ya serie A.

Hatua ya Wenger kutamka hayo inafuatia tetesi zilizozagaa kwa sasa nchini England zinazosema kuwa Joe Hart yu njiani kurejea katika Ligi ya premier kwa kujiunga na Arsenal.

Lakini akikanusha tetesi hizo, Wenger amesema kuwa mlinda mlango huyo hayumo katika mpango wake wa usajili wa majira ya kiangazi.

“Sina mpango wa kumsainisha Joe Hart ingawa kuna taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii.”

“Hayumo katika orodha ya wachezaji ninaowahitaji katika dirisha lijalo la usajili kwasababu sio chaguo langu kwa sasa.”


“Nina makipa watatu wa kiwango cha dunia, ninafarijika na uwepo wao hapa kwa sababu ninawaamini,” alisisitiza Wenger ambaye amekuwa akishutumiwa na mashabiki wa klabu yake kwamba amekuwa kocha asie na malengo ya kutwaa mataji ya ndani na nje ya England. 

No comments