Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: KUNA FUNZO KUBWA KWA WASANII NYUMA YA ‘LIST’ YA MAKONDA

on

Wiki chache zilizopita nilimsikia msanii mmoja wa kizazi kipya
akihojiwa radioni na kijisifia kuwa siku hizi hatumii kilevi chochote na kwamba
bangi alivuta zamani. Nilishangaa sana.
Nilishangaa kwakuwa msanii ni kioo cha jamii na kuna watoto wengi
ambao wanatamani kuwa kama yeye, hivyo kukiri kuwa zamani alivuta bangi
kunaweza kuwa kichocheo cha kuharibu mitazamo ya watoto hao wakiamini kuwa
kujaribu kuvuta bangi na kisha kuacha hapo baadae si jambo baya …ni jambo la
kifahari. Kwangu naamini msanii yule kusema hatumii kilevi ingetosha.
Kuuza na kuvuta bangi yote ni makosa, haijalishi ulivuta lini au kuuza
lini. Kukiri hadharani kuwa aliwahi kuvuta bangi ingetosha kabisa kwenda
kuisadia polisi. Wasanii wanadekezwa sana na ndiyo maana upuuzi kama huo hautoweki
miongoni mwao.
Majuzi mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitaja orodha ya
watuhumiwa wa uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya maarufu kama “Unga”.
Ndani ya orodha hiyo yalikuwepo majina ya wasanii kadhaa.
Nikiwa kama shabiki mkubwa wa muziki wa dansi na taarab, nilifarijika
sana kuona hakuna msanii wa dansi au taarab katika orodha ile, lakini bado niko
na tahadhari kubwa kuwa majina zaidi ya wasanii yataendelea kutajwa hivyo
lolote linaweza kutokea siku za usoni.
Sitaki kuwahukumu wasanii waliotajwa kuwa ni wauzaji au watumiaji wa
madawa ya kulevya lakini nashawishika kuamini kuwa wengi wao wameponzwa na
‘upumbavu’ wa maisha yao binafsi. Kutokujitambua, kutojiheshimu na
kujifaharisha kwa mambo ya kijinga kunahusika sana katika kuwafanya baadhi ya
wasanii wakae ki-unga unga… kama si uuzaji basi kuutumia.
Wasanii wengi wanasahau kuwa wao si binadamu wa kawaida, ni watu wa
kipekee, wanasahau kuwa wana nguvu kuliko hata wanasiasa, wanasahau kuwa kuna
maelfu ya watu wanatamani kuwa kama wao. Badala ya kujiheshimu ndio kwanza
wanafanya mambo ya ovyo uraiani na mwisho wa siku umaarufu wao unaporomoka na
hatimaye kipato kupungua.
Wewe ni mwimbaji, tena wa hali ya juu unayekubalika kila kona ya nchi,
lakini badala ya kutunza sauti yako unakesha kwenye ma-bar, unachafua meza kwa
vileo vya kila aina. Kwa kipato kipi? Kipato cha kazi yako kinajulikana, lakini
kwa fujo unazofanya za matumizi yasiyolingana na kipato chako usishangae siku
moja ukitajwa kama muuza unga …Unalewa kupindukia iwe ni wakati upo jukwaani au
hata nje ya jukwaa, taswira yako ni ya kilevi tu, kwanini watu wasikudhanie kuwa
unabwia unga?
Msanii unakuwa kiguu,  kila show upo, hata isiyokuhusu wewe upo
tu, unazurura ukumbi mzima, unafanya vituko vya kila aina, unaonyesha ufahari
wa kugida pombe kwa mashabiki ambao wangetamani zaidi kukuona jukwanii.
unategemea nini kama si kuhusishwa na orodha kama hiyo ya Makonda?
Wasanii wa dansi na taarab wana kazi kubwa ya ‘kuji-brand’ vinginevyo
wataendelea kula vumbi kwa kuamini kuwa umaarufu unalindwa kwa kuwa kiguu na
njia kwenye bar na kwenye vijiwe vya shisha au gomba. Imekula kwenu.
Msanii unapiga pombe hadi saa 10 za afajiri halafu ndio unakwenda
kulala, hupatikani kwenye simu hadi saa 11 jioni. Umewahi kujiuliza umepoteza
‘dili’ ngapi katika muda huo uliolala huku ukiwa hupatikani hewani?
Mwanamuziki unakuwa na rundo la wapambe ambao hawajui A wala B ya
muziki, kazi yao kubwa ni kuhakikisha ‘wanakuchuna’ pombe na kutengeneza
umaarufu uchwara kupitia jina lako, halafu bado unategemea ukue kisanii. Sahau
hiyo kitu.
Hakuna mpambe atakayekushauri kunywa pombe nyumbani, ataonekana vipi
kuwa yuko na supastaa kama mtaishia kunywa nyumbani? Mpambe ni lazima
akuchochee kwenda bar ili akauze sura na msanii mkubwa. Ipo haja ya kuwa makini
na uchaguzi wa marafiki.
Unapokaa kwenye onyesho lako huku meza yako na wapambe wako imechafuka
kwa pombe, unategemea nini kwa mshabiki wako aliyelipa kiingilio kuja kukuona?
Ni lazima mshabiki huyo atakudharau na mwisho wa siku atakacha kuja kwenye
maonyesho yako. Hasara iliyoje kwa mshabiki kukukimbia kwasababu ya maisha yako
ya kibwege ambayo ungeweza kuyamalizia nyumbani kwako.
Tatizo kubwa la wasanii wetu wengi ni shule ndogo na ni kama vile
hawakutegemea kuwa hapo walipo, haikuwa ndoto waliyoisaka kwa udi na uvumba na
ndio maana hawana muda wa kuyalinda mafanikio yao… wanaishia kuwa malimbukeni
na mazumbukuku. Hakika kuna funzo kubwa nyuma ya orodha ya Makonda, bila shaka
tutashuhudia mengi.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *