BEKI JORDI ALBA WA BARCELONA AMKINGIA KIFUA LUIS ENRIQUE... asema ni kocha bora licha ya kuandamwa na shutuma

BEKI mahiri wa timu ya Barcelona, Jordi Alba amemkingia kifua kocha wake Luis Enrique akisema kuwa anavyoamini ni bora licha ya kuandamwa na shutuma.

Enrique alianza kuandamwa kutokana na kipigo cha Barca cha mabao 4-0 dhidi ya Paris Saint-Germain katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa hatua ya 16 bora na huku mwishoni mwa wiki ikishuhudiwa wakihitaji bao la mkwaju wa penati dakika za mwisho katika mchezo dhidi ya timu inayokaribia kushuka daraja Leganes ili kuweza kupata ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa La Liga.

Hata hivyo, pamoja na matokeo hayo, Alba anaonyesha imani kubwa kwa Enrique ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

“Ni kati ya makocha bora ambao kwa sasa Barca inao,” alisema Alba.


Mbali na kumkingia kifua kocha huyo Alba vilevile alijipa matumaini kuwa watazinduka katika mchezo wa marudiano dhidi ya PSG ambao utapigwa Machi 8, katika uwanja wa Camp Nou.

No comments