EMMANUEL ADEBAYOR APATA "MAISHA" UTURUKI

HATIMAYE mshambuliaji wa kimataifa wa Togo, Emmanuel Adebayor amepata timu ya kuchezea baada ya kusugua benchi kwa muda mrefu.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal, Manchester City na Tottenham amesajiliwa katika timu ya Basaksehir ya Uturuki kwa mkataba wa miezi 18.

Habari ambazo zimechapishwa kwenye mtandao wa kijamii toka juzi zimesema kwamba klabu hiyo ya Istanbur Basaksehir imempa mkataba wa muda huo Adebayor kama mchezaji huru.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32 sasa amekuwa nje ya uwanja tangu alipoondoka katika klabu ya Crystal Palace katika mwisho wa msimu wa 2015/16.

Na sasa mchezaji huyo ambaye alikuwa kwenye fainali za Mataifa ya Afrika nchini Gabon akiwa na timu yake ya taifa ya Togo, ameangukia katika klabu hiyo ya Uturuki katika mkataba utakaomweka huko hadi Juni mwakani.

“Kabla ya kusaini mkataba huu, nilikuwa nimefanya mazungumzo na watu mbalimbali katika klabu hii na wakanihakikishia kwamba wananihitaji na ndio maana nimeamua kusaini,” amesema Adebayor.


“Nafurahi kwamba nimekuwa mmoja wa wachezaji wapya wa klabu hii na nimekuja hapa kuwafungia mabao. Nitafanya hivyo kama nilivyofanya wakati nikiwa Metz, Monaco, Arsenal, Manchester City, Real Madrid na Tottenham kisha Palace,” alisema mchezaji huyo.

No comments