GUARDIOLA AIKATIA TAMAA MANCHESTER CITY MBIO ZA UBINGWA ENGLAND

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Pep Guardiola amesema bado hajaridhishwa na kiwango cha kikosi chake na kumfanya akate tamaa ya kuwemo katika mbio za ubingwa wa premier kwa msimu huu.

Kisha akashangazwa na baadhi ya wadau wa soka duniani walioanza kuamini kuwa huenda msimu huu ungefanikisha azma ya klabu yake hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya nchini England pamoja na Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Guardiola ambaye ni kocha aliyepewa heshima kubwa na wadau wa soka walioamini kuwa ametua Manchester City kwa ajili ya kuendeleza historia aliyoiacha nchini Hispania alipokuwa na Barcelona na Ujerumani alipoiwezesha Bayern Munich kulitawala soka la Bundesliga.

Lakini katika mazingira yanayoonyesha kukata tamaa, kocha huyo alisema bado anaangushwa na kiwango cha wachezaji wake na kupata ushindi unaofanana na homa ya vipindi kwa kupanda na kushuka katika msimamo wa Ligi ya premier.

Akinukuliwa, Pep alisema alitegemea hali kama hiyo ya kutoanza vyema ni kutokana na kila timu kuiangalia Manchester City kwa jicho la ushindani wa kupitiliza.

Alisema, kadri muda unavyokwenda, haoni kama kuna dalili ya kikosi chake kupambana kwa ajili ya ubingwa na kwamba hajui sababu ila anaendelea ila anawashangaa wanaodhani kuwa timu yake bado imo kwenye ushindani uliotarajiwa awali.
“Sikubaliani na matarajio ya wadau wengi wa soka kuhusu kikosi changu kuwa miongoni mwa wanaofikiriwa kuwa mabingwa kwa msimu huu, bado hatujawa sawasawa kama ninavyotaka.”


“Ni vigumu kwa msimu wa kwanza kufanya maajabu kama ya kutwaa ubingwa katika Ligi ngumu kama ya England, pia katika Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kuna changamoto kubwa ya kuwepo kwa klabu zenye vikosi vyema, uwezo mkubwa na vilivyokaa kwa muda mrefu tofauti na Man City ambayo kwa sasa inajitengeneza,” alisema Guardiola.

No comments