HATUMWI MTOTO DUKANI USIKU WA ISHA MASHAUZI ALHAMISI HII MANGO GARDEN


ZIKIWA zimesalia siku chache kutimia tarehe 9 Februari, habari moja tu …Usiku wa Isha Mashauzi (Isha’s Night) utakafanyika ndani ya Mango Garden Kinondoni Alhamisi hii.

Onyesho hili ambalo hufanyika kila mwaka, linasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa taarab na muziki kwa ujumla hasa kwa namna ambavyo Isha huwa hakoseagi katika siku yake hiyo maalum.

Kama ilivyosemwa hapo awali, ni onyesho ambalo humpa nafasi Isha Mashauzi kusherehekea siku yake ya kuzaliwa huku akipewa uwanja mkubwa wa kuonyesha uwezo wake wa kukamua jukwaani kwa muda mrefu bila kupumzika.

Naaam, ni usiku ambao Isha Mashauzi husimama jukwaani kwa zaidi ya saa mbili mfululizo na kupiga nyimbo zake zote kali.

Kwa mara nyingine tena Isha ataimba zaidi ya nyimbo nane mfululizo kitu ambacho hakijawahi kufanywa na mwimbaji yoyote wa taarab, awe wa kiume au wa kike.

Mbali na Isha Mashauzi na bendi yake ya Mashauzi Classic, Ishas’s Night itasindikizwa na Siza Mazongela pamoja na Kibao Kata.

Hapo nyuma, Isha Mashauzi aliiambia Saluti5 kuwa siku hiyo pia itakuwa ni maalum kwa wote waliozaliwa mwezi Ferbruari “Team Februari” na kwa sasa anaendelea kusisitiza kuwa Team February  wafike kwa wingi wakiwa na watu wao muhimu ili kupata ile kitu roho inataka.No comments