JERMAIN DEFOE ASEMA HANA MPANGO WA KUACHANA NA SOKA KWA SASA

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Sunderland ya Uingereza, Jermain Defoe amesema kwamba hana mpango wa kuachana na soka kwa wakati huu.

Nyota huyo amesema kwamba amekuwa akipata shinikizo kutoka kwa mama yake mzazi akimtaka aachane na soka lakini yeye anaona kwamba muda bado.

Defoe mwenye umri wa miaka 35, ameifungia Sunderland mabao 14 msimu huu katika mechi 24 alizoshuka uwanjani na amesema anataka aendelee kufunga zaidi.

“Kuna watu wanatamani kuniona nimeachana na soka, hata mama yangu mzazi anataka kuniona nikipumzika kucheza soka. Lakini najiona nina nguvu kama kijana mwenye miaka 18 hivi, nataka niendelee kung’ara na ndio maana unaona timu nyingine zinanitaka pia,” amesema.

Defoe ambaye alijiunga na watemi hao wa dimba la Wearside akitokea Toronto mwezi Januari, mwaka juzi wa 2015, ameongezewa miezi 12 zaidi katika mkataba wake kwenye klabu hiyo.


Kutokana na makali yake, baadhi ya klabu ikiwemo waajiri wake wa zamani, West ham United wamejaribu mara kadhaa kutaka kumrejesha kikosini hapo.

No comments