KOCHA OMOG ATAMBA KUIPA SIMBA UBINGWA WA LIGI KUU MSIMU HUU

LICHA ya kwamba Simba imebakiza mechi saba kumaliza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu wa 2016/17, kocha wa wekundu hao wa Msimbazi, Mcameroon Joseph Omog ameahidi kuipa ubingwa wa Tanzania Bara hata kama atateleza mchezo mmoja.

Omog anaamini Simba itachukua ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu kutokana na msingi imara alioujenga tangu mwanzo wa msimu.

Mcameroon huyo alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akichukua mikoba ya Mwingereza Dylan Kerr.

Kerr alikuwa akiinoa Simba lakini akatimuliwa baada ya kushindwa kufikia malengo ya Wanasimba, nafasi ya Mwingireza huyo ilikaimiwa kwa muda na Mganda Jackson Mayanja ambaye sasa ni msaidizi wa Omog.

Kocha huyo mwenye rekodi ya kuvutia akiipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho barani Afrika timu ya FC Leopards ya Congo Brazaville, pia akaipa ubingwa wa Tanzania Bara timu ya Azam FC aliyoiongoza kwa msimu mmoja, Simba wakaridhishwa na rekodi hiyo na ndio maana wakampa mkataba wa miaka miwili.

“Matarajio yangu ni kuipa ubingwa Simba msimu huu, tuna kikosi kizuri na sidhani kama tunaweza kushindwa hata kama tutateleza mchezo mmoja,” alisema Omog ambaye si mzungumzaji sana kama walivyo makocha wengi wa Kiafrika.

No comments