KOCHA WA NDANDA FC ASEMA “SINA SHAKA TUTABAKI TU LIGI KUU”

UMEMSIKIA kocha wa Ndanda FC “Wana Kucheele” ya Mtwara, Meja mstaafu Abdul Mingane, jamaa anasema hesabu zao bado zinawapa matumaini ya kubakia Ligi Kuu.

Ndanda ni kati ya timu zinazopigania pumzi ya kubakia Ligi Kuu Tanzania bara, lakini yeye amekataa kuzima matumaini ya kubaki.

Amesema ikiwa watashinda mechi tatu au nne kati ya zilizosalia, jambo ambalo anaamini linawezekana, hawatashuka daraja.

Kocha huyo alisema kuwa aliitwa kwa ajili ya kuokoa jahazi hilo lisizame na kutokana na mwenendo wa Ligi ulivyo anajipa matumaini makubwa ya kuibakisha Ndanda katika Ligi Kuu.

Hata hivyo, ameonya tabia ya viongozi wa timu hiyo kuacha tabia ya kubadili makocha kila kukicha ikiwa wanataka kupata mafanikio ya kisoka.


“Mimi jambo moja ambalo nadhani uongozi unatakiwa kujifunza kwamba mafanikio hayaji kwa haraka, hivyo wanatakiwa wakubali kudumu na kocha kwa muda mrefu badala ya kuwa na kocha mpya kila baada ya msimu au miezi michache, kupoteza mchezo mmoja au miwili sio sababu ya kufukuza kocha,” alisema.

No comments