VIRGIL VAN DIJK AIWEKA ROHO JUU KLABU YAKE YA SOUTHAMPTON

WASIWASI umeendelea kutanda ndani ya klabu ya Southampton juu ya mlinzi wao kisiki, Virgil van Dijk ambaye taarifa zinasema anatakiwa na timu mbalimbali barani Ulaya.

Shaka iliyopo ni kwamba Van Dijk anaitumikia katika hatua ya mwisho klabu yake hiyo huku taarifa kuu zikisema anawaniwa na Chelsea, Manchester City na Barcelona.

Magazeti nchini England yamebainisha kuwa beki huyo ana mawasiliano na klabu ya Barcelona na kwamba mpango huo unaweza kukamilika katika kipindi cha usajili cha majira ya joto.

Van Dijk aliumia kifundo cha mguu wa kushoto wakati Southampton ikikipiga na Leicester City mnamo Januari 22, mwaka huu na tangu hapo hakuonekana tena dimbani.

Lakini taarifa zilizopo sasa zinasema kuwa Van Dijk atakuwemo katika kikosi cha kwanza cha Southampton inayotarajiwa kuumana na Manchester United katika mchezo wa fainali kuwania ubingwa wa Kombe la Ligi ya England Februari 26, mwaka huu.


Hata hivyo, wabashiri wa masuala ya soka wanaamini kuwa huenda mchezo huo ukawa wa mwisho kwa mlinzi huyo kwani tayari kuna klabu mbalimbali zinamwania kwa ajili ya usajili wa majira ya kiangazi.

No comments