WAYNE ROONEY AWEKA WAZI AZMA YAKE YA KUTOONDOKA OLD TRAFFORD

HII ndio kauli ya mwisho ya nahodha wa mashetani wekundu wa jiji la Manchester, Wayne Rooney ambapo amesisi tiza kubaki Old Trafford kwa miaka mingi ijayo.

Kisha akaweka bayana kuwa hata kama atahitaji kuondoka Manchester United, bado hafikirii kwenda kusakata soka kwenye klabu za nchini China na kwamba hilo litakuwa binafsi kuamua.

Kauli hiyo ya Rooney inakuja siku chache baada ya kuhusishwa kutaka kuondoka na kwenda kusakata kabumbu katika nchi hiyo ya mashariki ya mbali, yaani China.

Rooney ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya England, amenukuliwa akisema mipango yake ni kuendelea kusakata soka ndani ya United sambamba na timu yake ya taifa na si vinginevyo kwa sasa.

Nahodha huyo mwenye umri wa miaka 31, amesisitiza kuwa lililo ndani ya fikra zake hivi sasa ni kuisaidia United kupambana kwa ajili ya ubingwa wa primier pamoja na kusaka nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

“Bado nina majukumu ndani ya United ambayo nitayakamilisha katika miaka mingi ijayo, hivyo bado nipo hapa kwa muda mrefu.”

“Ninawaomba radhi wale wote waliosumbuka kutokana na taarifa za mimi kuondoka hapa. Nadhani ni mambo ya uvumi ambao mimi ndie ninayepaswa kuumaliza.”

“Ni wakati wa furaha kubwa katika klabu hii na ningependa kusalia,” alisema Rooney.

Taarifa za ndani zilisema kuwa Rooney alikuwa akitajwa kwenda nchini China kujiunga na kati ya timu mbili za huko ambazo ni Beijing Guoan na Jiangsu Suning.

No comments