AGGREY MORRIS AELEKEZA AKILI YAKE KWENYE MECHI DHIDI YA YANGA JUMAMOSI HII

BEKI wa timu ya Azam, Agrey Morris ambaye ameanza mazoezi mepesi baada ya kupata majeraha ya mfupa wa paja, amesema kwamba akili yake inafikiria mchezo wao mgumu unaofuata dhidi ya Yanga katika dimba la uwanja wa taifa.

Morris alilazimika kuwa nje ya kikosi baada ya kupata majeraha ya paja katika mchezo wa kimataifa dhidi ya Mbabane Swallows ambapo Azam ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

“Hakuna mchezaji anayependa kukaa nje ya kikosi kwani kazi yetu ni kucheza mpira, hivyo namshukuru Mungu kwakuwa nimeanza mazoezi uwanjani na kikosi cha kwanza baada ya kumaliza program ya gym.”

“Naamini nitakuwa fiti kuikabili Yanga katika mchezo wa marudiano ambao hatupaswi kuupoteza ili kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara,” alisema Morris.

“Yanga ni timu ngumu iliyosheheni nyota wenye uzoefu wa Ligi lakini kwetu sisi ushindi ndio kila kitu bila kujali ukubwa wa majina ya wachezaji wao.”

Mara ya mwisho klabu hizo zilikumbana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo Azam walifanikiwa kuifunga Yanga kwa jumla ya mabao 4-1, hivyo mtanange ujao utakuwa na taabu kwa  miamba hiyo ya Dar es Salaam kukutana.


Klabu ya Yanga ambayo imeachwa pointi mbili na Simba katika msimamo wa Ligi, nayo inalazimika kucheza kufa nba kupona ili kuzidi kuwapa presha wekundu wa msimbazi ambao wako kileleni hivi sasa.

No comments