Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: BENDI ZETU ZINAFANYA JUHUDI ZA KUZALISHA MASHABIKI WAPYA?

on

Siku fulani hapo zamani kidogo mtangazaji Salma Msangi wa 92.9 Magic
FM kupitia kipindi cha Afrika Kabisa, alizungumza kitu ambacho kiliwachoma
wadau na wanamuziki wengi dansi – alisema muziki wa dansi UMEKUFA!
Salma akahoji ni vipi wao watangazaji waupige muziki ambao hautakiwi
tena na mashabiki. “Watu hawautaki tena muziki wa dansi …muziki wa dansi
umekufa,” alisikika mtangazaji huyo na kuwataka wasanii wa dansi waache
kulalamika na badala yake wasome alama za nyakati.
Katika kusheresha kauli yake, Salma Msangi akampongeza Christian Bella
kwa kusoma alama za nyakati na kuamua kushirikiana na wasanii wa bongo fleva
kama Ommy Dimpoz na wengineo na sasa yuko juu.
Huo ni mtazamo wa Salma Msangi na sitaki kuwa hakimu kwenye kauli yake
– anaweza kuwa sahihi au si sahihi, anaweza kuwa ametumia njia sahihi
kuzungumzia hilo lakini pia anaweza kuwa ametumia njia ya kuumiza na kukatisha
tamaa ila yote kwa yote hayo ni maoni ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi kwani
pengine yapo mawili matatu yanayofaa katika safari ya kuukwamua muziki wa
dansi.
Kwangu mimi naamini muziki wa dansi haujafa bali unazidi kukua kwa
kasi ya ajabu kiasi cha kujipenyeza kwenye aina nyingine ya muziki kama vile
bongo fleva, taarab na injili – ukifuatilia kwa makini aina hizo nyingine za
muziki utagundua kuwa kwa zaidi ya asilimia 40 wanautegemea sana muziki wa
dansi.
Majuzi mwanangu wa kidato cha tatu alinikuta natazama wimbo “Yarabi
Nafsi” wa Mapacha Watatu katika laptop yangu kupitia YouTube, akashangaa sana
na kuniuliza: “Hivi kumbe hata muziki wa bendi unapatikana You Tube?” Nikamjibu
kwa kumhoji: “Kwanini ulifikiri haupatikani?”.
Akanijibu: “Kwa sababu najua watu hawapendi muziki wa bendi za dansi,
hawatapata viewers (watazamaji) wengi.” Kuthibitisha hilo akasogelea laptop
yangu na kuangalia wimbo umepata watazamaji wangapi, akakuta 2781 akacheka na
kuniambia: “Si umeona watazamaji hao, sasa nenda kwenye video zingine za bongo
fleva au comedy uangalie ‘viewers’ utakuta ni elfu 50 na kuendelea,”.
Kwa bahati nzuri wakati dogo anayasema hayo nilikuwa na rafiki yangu
mmoja, tukatazamana na kutabasamu kwa uchungu, ulikuwa ni ukweli unaoumiza
kutoka kwa kijana mdogo ambaye ambaye anawakilisha sehemu ya kizazi kikubwa
kinachoamini kuwa muziki wa dansi kupitia bendi zetu haukubaliki.
Na ni hapo ndipo ninapojiuliza je bendi zetu zinajua kuwa zinahitaji
kuzalisha mashabiki wapya kwa maana ya kizazi kipya? Mashabiki wanazeeka kiasi
kwamba inafika wakati watu wanashindwa kwenda kwenye kumbi za starehe, nani
anaziba nafasi zao? Watangazaji na waandishi waliokuwa wakiunadi muziki wa
dansi miaka 20 iliyopita leo hii hawapo tena – wengine wamestaafu, wengine
wamefariki, wengine wamebadilishiwa majukumu na sasa zimekuja damu mpya. Je
bendi zetu zimefanya juhudi za kuishawishi jamii mpya ya wana habari?
Wanamuziki nao wanapotea mmoja mmoja huku wakikosa warithi – kila damu
msanii mpya wa muziki anakimbilia kwenye bongo fleva na mbaya zaidi kila mmoja
anataka kuwa mwimbaji. Hakuna anayetaka kujifunza kupiga chombo chochote na
haitashangaza miaka 20 ijayo Tanzania ikawa haina mpiga gitaa wala ngoma.
Nadhani alichopaswa kusema Salma Msangi ni kuwa muziki wa bendi za
dansi UNAKUFA. Bendi zimekosa ubunifu wa kwenda na wakati, ziko bendi zinapiga
aina ile ile ya muziki kwa zaidi ya miaka 10, 15 au 20 bila kujali kuwa soko la
muziki linabadilika kila wakati na kwamba walilazimika kulifuata.
Inauma sana unaposikiliza vipindi vya muziki wa kiafrika kama Weekend
Bonanza, Afrika Kabisa, Afro Power, Buzuki, Tanzania Stars, Afro Rhythm na
vingine vingi, vinapopiga nyimbo za wasanii wa bongo fleva badala ya muziki wa
bendi kama ilivyotarajiwa na wengi.
Lakini utawalaumu vipi watangazaji na waandaji wakati bendi zetu
hazitaki kubadilika, hazitaki kurekodi nyimbo mpya na wala hazitaki kujiuliza
ni kwanini nyimbo binafsi za wasanii wao zinapata muda wa kutosha redioni huku
za bendi zinadorora.
Kama msanii wa bendi anaweza kutoa wimbo wake binafsi unaokidhi
mahitaji ya soko na ukapigwa redioni. ni kwanini asifanye hivyo kwenye bendi
yake? Ni wazi kuwa fikra zao hazikubali ndani ya bendi na hivyo wanaamua kutoka
kivyao vyao.
Kumbi zinazidi kukauka mashabiki, watu wanakimbilia ‘club’ kucheza
disco au muziki wa kizazi kipya, inafika wakati hata bendi zinazopiga bure
kwenye bar hazipati mashabiki – hiyo ni dalili tosha kuwa muziki wa bendi za
dansi unakufa na kama juhudi za kuzalisha mashabiki wapya hazitafanyika, basi
‘mauti’ kwa bendi zetu yatakuwa hayakwepeki.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *