AYA 15 ZA SAID MDOE: IPO SIKU MUZIKI WA DANSI UTAGEUZWA KUWA KIROBA


Agizo la kupiga marufuku pombe kali zilizohifadhiwa katika mfumo wa pakiti ndogo ndogo (viroba), limepokewa kwa mzuka na baadhi ya watendaji ambao wengi wao wamejaribu kutuaminisha kuwa viroba ni hatari kwa afya na zina madhara mengi kwa matumizi ya mwanadamu.

Yaani ni kama vile kilichomo ndani ya kiroba ndicho kilichokatazwa na sio kifungashio – baadhi ya watendaji wanasahau kuwa kilichopigwa marufuku ni kifungashio na si kilichomo ndani.

Serikali iliweka wazi kuwa vileo hivyo vinapaswa kuhifadhiwa kwenye mfumo wa chupa tena kwa ujazo wa juu na wa bei ya juu na kukemea uuzaji wa kiholela ulipolekea baadhi ya watoto wa shule kuwa wateja wa viroba. Kwa serikali tatizo ni kifungashio lakini sio kilichomo ndani ila baadhi ya watendaji wanatamka vitu vinavyopingana na ukweli wa zoezi lenyewe.

Zoezi la kukataza viroba nalifananisha na la mabadiliko ya muziki wa dansi yanayopigiwa kelele na wadau wengi wa muziki.


Hofu yangu ni kwamba tunakoelekea tunaweza kujisahau na kusema muziki wa dansi haufai, uachwe na badala yake tukomae na bongo fleva na singeli. Watu wakadhani tatizo ni kilichomo ndani na si kifungashio.

Kinachopaswa kubadilishwa ni kifungashio cha muziki wa dansi na si kuufuta kabisa. Unawezaje kuufuta muziki wa dansi ambao ndiyo muziki ‘baba’ hapa nchini? Unaufutaje katika kipindi hiki ambacho hata nyimbo ya bongo fleva haikamiliki bila kutiwa mkono na msanii wa dansi?

Unaufutaje muziki wa dansi wakati nyimbo zote za taarab za hivi sasa zinapambwa na muziki wa dansi ndani yake? Vipi kuhusu muziki wa injili? Hakuna dansi ndani ya muziki wa injili?

Bahati mbaya sana kwa muziki huu ni kwamba unapita kwenye miluzi mingi sana, miluzi ile ambayo tunaambiwa ikizidi humpoteza mbwa. Kila mmoja anasema lake …wako wanaotaka dakika zipunguzwe (nyimbo ziwe fupi), wako wanaotaka magitaa yasipewe kipaumbele, wengine hawataki masebene achiliambali wale wanaotaka dansi iige kila kitu cha bongo fleva.

Muziki wa dansi wala hauhitaji mageuzi makubwa, ni kiasi tu cha kuboresha tungo na kuacha kurefusha nyimbo bila sababu za msingi, kuachana na mtindo wa kutaja majina mengi ya wadau, jambo ambalo halina maana yoyote zaidi ya kuchafua tu nyimbo.

Kuna maadui wawili wa muziki wa dansi: Adui wa kwanza ni wale wanaotaka dansi iwe kama bongo fleva. Hawa dhamira yao ni moja tu – kuua na kuufuta kabisa muziki wa dansi.

Adui wa pili wa muziki wa dansi ni wanamuziki wenyewe wa dansi kwa kukubali kwao kuwa watumwa wa muziki wa Congo (Zaire) kwa miaka nenda rudi. Kila kinachobadilika Congo basi na Tanzania lazima ifuate mkumbo.

Congo walipoanza kuondoa ala za upepo kama trumpet na saxophone nasi tukaiga, walipoingia kwenye mwendokasi (soukous), hatukubaki nyuma tukaiga, zile rap za Congo zilizoanzishwa na kina Bileku Mpasi na wengineo tukaiga pia, hata tabia ya kutaja utitiri wa majina ya wadau na mapedeshee nayo tumeiga kwao. Kwa kifupi kioo chetu kimekuwa ni muziki wa Congo. Tumeiga kila aina ya mitindo yao, kila aina ya uchezaji wao.

Sasa hivi baadhi ya nyota wa Congo wameanza kubadilisha muziki wao na kukimbilia soko la Kinigeria, tayari na huku tumeanza kuambiwa tupige dansi kwa mapigo ya Kinigeria. Yaani hatuwezi kabisa kubuni chetu.

Hiki ni kilema kikubwa sana Tanzania na ndiyo maana hata bongo fleva wakati fulani ilikuwa mtumwa wa muziki wa Afrika Kusini kabla ya kuhamishia ‘wizi’ wao kwa muziki wa Kinigeria …bongo movie wamekuwa watumwa wa filamu za Kinigeria kama huamini jiulize huu mfumo wa filamu za part 1 na 2 umetokea wapi.

Tuutukuze muziki wa dansi, tuujaze kwa vionjo vya ngoma zetu za asili ili tupate utambulisho (idetinty) yetu. Tusikubali kuwa bendera kufuata upepo, kinachopaswa kufanyika katika muziki wa dansi ni maboresho (kifungashio) ambayo hayataondoa misingi ya muziki wa dansi na ndiyo maana nasisitiza tatizo ni kifungashio na si kilichomo ndani ya kifungashio.

No comments