Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: WAIMBAJI WA DANSI WA KIUME SASA VUENI UHUSIKA WA KIKE

on

Majuzi nilikuwa nimekaa na mwangu huku nikisikiliza wimbo wa zamani “Gama”
wa DDC Mlimani Park “Sikinde” ambao ndani yake mwimbaji Cosmas Chidumule anavaa
uhusika wa kike na kumwaga malalamiko makubwa ya mwanamke kwenda kwa mumewe.
Mwanangu akaniuliza mbona huyu anayeimba ni mwanaume lakini
anamlalamikia ‘mumewe’? Nikacheka na kumwambia zamani kulikuwa na uhaba wa
waimbaji wa kike kwahiyo hapa msanii anajaribu kuvaa uhusika wa kike ili
kuwasilisha ujumbe. Akanikubalia kwa shingo upande.
Zamani ilikuwa kitu cha kawaida sana kumsikia mwimbaji mwenye sauti
nzito kama marehemu Dr Remmy akiimba wimbo “Mume Wangu”.
Ndani ya wimbo huo Dr Remmy akavaa uhusika wa kike kiasi cha kukujaza
hisia msikilizaji mpaka ukahisi kuwa unamsikiliza mwanamke ‘halisi’ akitema
machungu yake juu ya mumewe.
Waimbaji wengi wa zamani wamefanya hivyo, hata Marijan Rajab, Hemed
Maneti, Adam Bakari, Bitchuka, Dede na wengine kadha wa kadha.
Hata nchi jirani  Zaire (DRC)
magwiji kama kina Luambo, Tabu Ley, Pepe Kalle nao pia wamewahi kuimba nyimbo
zilizowalazimisha kuvaa uhusika wa kike.
Siwalaumu sana waimbaji waliofanya hivyo kwa kuwa hakuna ubishi kuwa
enzi hizo kulikuwa na ukame wa waimbaji wa kike wa dansi.
Kingine kilichochangia hali hiyo ni ile imani kuwa waimbaji wa kike ni
wasumbufu, imani ambayo inaendelea hadi leo hii na ndiyo maana katika kila
bendi 10, basi yenye mwimbaji wa kike ni moja huku tisa zikiwa za wanaume
watupu.
Lakini dunia inakimbia kwa kasi sana, watu wanaerevuka kwa kasi ya
ajabu na hivyo imefikia hatua ambayo sasa mwanaume ukiimba kwa kuvaa uhusika wa
kike unaonekana kituko.
Ifike mahali sasa waimbaji wetu waachane na tabia hiyo na tulazimike
kutumia waimbaji wa kike hata wa ‘kuazima’ pale panapohitaji kuimbwa kwa nafsi
ya kike.
Bado kuna nyimbo kadhaa za sasa hivi kutoka kwa bendi zetu ambazo
zinaendelea kutumia mfumo huo wa waimbaji wa kiume kuvaa uhusika wa kike, jambo
ambalo kwa mazingira ya sasa linapunguza uhalisia wa ujumbe unaowasilishwa.
Nadhani licha ya bongo fleva kupambwa na mambo mengi machafu mchafu,
lakini waimbaji wa dansi wanapaswa kujifunza vitu fulani kwa wasanii hao wa
kizazi kipya. Vipo baadhi vitu vyao vimekaa kisasa na kisomi.
Siamini kuwa kuna siku Diamond au Ali Kiba anaweza kuimba nyimbo
yoyote kwa kuvaa uhusika wa kike. Katika dunia ya leo ambayo imezungukwa na
janga ‘mashoga’ haipendezi tena mwanaume kuimba kwa kuvaa uhusika wa kike.
Kama amekosekana mwimbaji wa kike na kuna ujumbe unahitajika
kuwasilishwa kupitia nafsi ya kike, basi ni bora mwimbaji wa kiume aimbe kwa
nafsi ya tatu …kwa staili ya kusimulia kile alichofanyiwa mwanamke.
Yaani badala ya mwanaume kuimba “Nimechoka mimi na mwanaume mlevi heri
anipe talaka nirudi kwetu …” basi aimbe “Amechoka yeye na mwanaume mlevi heri
umpe talaka arudi kwao …” Mfano mzuri wa tungo hizi ni “Kisa cha Photo Album”
wa JKT Kimulimuli chini ya Zahir Ally Zoro ambao kwa alisimia 80 malalamiko ya
mwanamke yaliwasilishwa bila mwimbaji wa kiume kuvaa uhusika wa kike.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *