FABREGAS AZIDI KUSISITIZA "KANTE NI BONGE LA KIUNGO ANAYESTAHILI SIFA NYINGI ZAIDI YA HIZI"

KIUNGO Cesc Fabregas amesisitiza kuwa mchezaji mwenzake wa Chelsea, N’Golo Kante ni kiungo aliyekamilika na anastahili sifa nyingi zaidi ya anazopata kwa sasa.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa amepigiwa chapuo kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa PFA mwisho wa kampeni hizi baada ya kuwa mhimili mkuu wa Blues katika mbio za ubingwa.

Kante alijenga sifa yake kama kiungo mwenye uwezo wa kuvuruga mipango ya wapinzani na kusambaza mipira kwa wenzake alipokuwa Leicester City, lakini Fabregas amesisitiza kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 ana uwezo wa kufanya makubwa zaidi ya inavyodhaniwa.

“Kwa bahati mbaya mchezo wa soka siku hizi unaendana na majukumu ya mchezaji,” aliiambia tovuti ya Chelsea.

“Sasa N’Golo Kante amekuwa maarufu kwa kukimbia kwa kasi, kukaba na kupokonya mpira na hatimae kufunga pia, lakini anafanya kila kitu vizuri.”

“Lakini kwa sababu hili ndio jukumu lake watu wanaona hilo tu na hawafuatilii mengine, nadhani tunashinda kama timu, tunachukia kupoteza lakini kila mmoja ni kiongozi wa timu na ndivyo ilivyo.”  


Kante amefunga goli lake la pili la msimu kwa Chelsea Jumatatu usiku katika mechi ya Kombe la FA walipotoka kifua mbele dhidi ya Manchester United kwa ushindi wa bao 1-0 na aliifunga United goli lake la kwanza Oktoba.

No comments